Kiongozi mpya wa kijeshi kuapishwa Madagascar Ijumaa
16 Oktoba 2025
Katika kauli aliyoitoa jana Jumatano Kanali Michael Randrianirina amethibitisha kuwa ataapishwa kuushika wadhifa wake mpya kama Rais wa Madagascar. Anatazamiwa kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha mpito cha hadi miaka miwili.
Itakumbukwa kuwa kiongozi huyo wa kijeshi alikuwa na jukumu muhimu katika kikosi maalumu kilichofanya mapinduzi mwaka 2009 na kumweka madarakani Andry Rajoelina. Hata hivyo katika maandamano ya hivi karibuni kikosi hicho kilimpa kisogo kiongozi huyo na kuamua kuwa upande wa wananchi ambapo kiliwataka polisi wasiwafyatulie risasi waandamanaji.
Maandamano hayo ya kuipinga serikali yake yalianzishwa na vuguvugu lililoongozwa na vijana maarufu Gen Z Septemba 25 wakilalamikia ukosefu wa maji na huduma za umeme. Mtawala mpya Kanali Randrianirina atakapoapishwa hapo kesho atawaongoza takriban watu milioni 30. Robo tatu ya raia hao wanaishi katika dimbwi kubwa la umasikini.
Umoja wa Afrika waivua uanachama wa Madagascar
Utawala mpya wa kijeshi unatazamiwa kuapishwa wakati Umoja wa Afrika umetangaza jana kuwa umeifuta Madagascar uanachama kutokana na mapinduzi yaliyomwondoa madarakani Rais Andry Rajoelina.
Umoja huo pia umetoa wito kwa taifa hilo kurejesha utawala wa kiraia na kufanya uchaguzi.Akizungumzia uamuzi wa chombo hicho Kanali Randrianirina amesema mapemaAlhamisi kwamba ni hatua iliyokuwa ikitegemewa na kwamba kuanzia sasa kutakuwa na mazungumzo ya faragha.
Kuondolewa kwa Madagascar katika Umoja wa Afrika kunabeba uzito kisiasa na kunaweza kuutenga utawala mpya. Wakati huohuo kwa mara ya kwanza Rais Andry Rajoelina amethibitisha kuwa aliikimbia nchi baada ya maandamano makubwa ya wiki kadhaa.
Rajoelina aliondoka kati ya Oktoba 11 na 12 baada ya kile ofisi yake ilichokiita kuwa "vitisho vikali dhidi ya maisha ya mkuu wa nchi". Hata hivyo ripoti za vyombo vya habari viliashiria kuwa kiongozi huyo mwenye miaka 51 aliondolewa nchini humo na ndege ya kijeshi ya Ufaransa.