Marekani: Ina taarifa juu ya mauaji ya Abu Firas al-Suri
4 Aprili 2016Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria, Rami Abdel Rahman, Abu Firas al-Suri alikuwa anakutana na wapiganaji wengine waliyo na itikadi kali, katika ngome ya Kafar Jales ya kundi la al Nusra Front wakati waliposhambuliwa.
Hata hivyo bado haijawa wazi iwapo mashambulizi hayo ya angani yalifanywa na ndege za kivita za kutoka serikali ya Syria au mshirika wake wa karibu Urusi.
Abu Firas al-Suri ambaye jina lake halisi ni Radwan Nammous, alipigana dhidi ya vikosi vya kisovieti nchini Afghanistan ambako alikutana na kiongozi wa Al Qaeda Osama bin Laden pamoja na mshauri wake Abdullah Azzam kabla ya kurejea nchini Syria mwaka wa 2011.
Marekani iliyokuwa ikipambana na kundi la Al Nusra Front kwa muda mrefu imesema inataarifa juu ya kuuwawa kwa Al Suri lakini haikuwa na taarifa zaidi za kutoa juu ya kifo chake.
Kando na hayo maeneo mengine yanayoshikiliwa na kundi hilo la Al Nusra Front na kundi jengine linaloshirikiana nalo la Jund al-Aqsa, Kaskazini mwa mji wa Idlib pia yalishambuliwa na kuwajeruhi wengi.
Mazungumzo juu ya hatima ya Assad huenda yakazuwiya upatikanaji wa suluhu la kisiasa.
Wakati huo huo makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano yaliyokubaliwa kati ya vikosi vya serikali na waasi yameendelea kuheshimiwa tangu tarehe 27 mwezi wa Februari, lakini makubaliano hayo hayawajumuishi makundi ya Al Nusra Front na kundi la wanamgambo wa dola la kiislamu.
Makubaliano hayo yameipa nafasi Urusi na muungano unaoongozwa na Marekani waliokuwa wanalishambulia kundi la IS nchini Syria, kuunganisha nguvu zao dhidi ya makundi ya jihadi.
Huku hayo yakiarifiwa shinikizo la kumtaka rais wa Syria Bashar al Assad kungatuka madarakani huenda ikazuwiya upatikanaji wa suluhu la kisiasa nchini humo, hii ni kwa mujibu wa shirika la habari la Urusi RIA lililomnukuu Naibu Waziri wa nchi za nje wa Urusi Sergei Ryabkov. Moscow imependekeza mazungumzo juu ya hatima ya Assad yasimamishwe huku ikisema suala hilo linapaswa kujadiliwa na kuamuliwa baadaye na pande husika katika mgogoro wa Syria.
Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miaka mitano Syria yamesababisha mauaji ya watu zaidi ya 270,000 huku mamilioni ya wengine wakiachwa bila makao na kundi kubwa likikimbilia barani Ulaya.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP
Mhariri: Yusuf Saumu