1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Al-Shabaab akamatwa Somalia

28 Desemba 2014

Kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab nchini Somalia, Zakariyah Ismail Ahmend Hersi, amekamatwa na polisi baada ya kujisalimisha jana Jumamosi (27.12.2014).

Wapiganaji wa Al-Shabaab nchini Somalia
Wapiganaji wa Al-Shabaab nchini SomaliaPicha: picture alliance / AP Photo

Afisa mmoja wa idara ya ujasusi amesema Hersi alijisalimisha kwa polisi katika mkoa wa Gedo, baada ya kile kinachoonekana ni uwezekano wa kuzuka mzozo ndani ya kundi hilo.

Huenda Hersi anatofautiana na wapiganaji watiifu kwa kiongozi wa Al-Shabaab, hayati Abdi Godane, aliyeuawa katika shambulio la anga lililofanywa na Marekani mwanzoni mwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, afisa wa kijeshi wa ukanda huo, Jama Muse, amesema Hersi alikuwa anasimamia masuala ya kijasusi na fedha na pia alikuwa ni mmoja kati ya makamanda waandamizi wa Al-Shabaab.

Kiongozi wa Al-Shabaab aliyeuawa, Ahmed Abdi GodanePicha: Rewards for Justice/AFPGetty Images

Ingawa jeshi la Somalia lilimuweka katika orodha ya mawakala wa Al-Shabaab, haijafahamika wazi iwapo Hersi bado alikuwa ana nguvu ndani ya kundi hilo la kigaidi katika miezi michache iliyopita. Inawezekana kuwa Hersi alikuwa miongoni mwa kundi la makamanda waliotofautiana na Godane kabla ya kifo chake.

Marekani iliahidi Dola milioni 3

Marekani iliahidi kutoa zawadi ya Dola milioni tatu ambazo ni sawa na Euro milioni 2.14, kwa mtu atakayefanikisha kukamatwa kiongozi huyo. Hata hivyo, wizara ya mambo ya nje haijazungumza chochote kuhusu taarifa hizo.

Kundi la Al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, limeendelea kuwa tishio nchini Somalia na Afrika Mashariki. Kundi hilo limefanya mashambulizi kadhaa ya kigaidi nchini Somalia na katika nchi jirani, ikiwemo Kenya, ambayo wanajeshi wake ni sehemu ya kikosi cha Umoja wa Afrika kinachokisaidia kikosi cha Somalia kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Siku ya Alhamisi ambayo ilikuwa ni sikukuu ya Krismasi, kundi la Al-Shabaab lilifanya mashambulizi katika kambi ya kikosi cha Umoja wa Afrika-AMISOM kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na kuwaua watu 14, wakiwemo wapiganaji wote wanane wa kundi hilo.

Makao makuu ya Kikosi cha AMISOM, MogadishuPicha: Getty Images/AFP/Mohamed Abdiwahab

Kundi hilo limekiri kuhusika na shambulio hilo ambalo lilikuwa la kulipiza kisasi kutokana na mauaji ya Godane, na kuharibu pia nyumba za maafisa wa Umoja wa Mataifa na balozi za mataifa ya Magharibi. Msemaji wa Al-Shabaab, Sheikh Mohamud Rage, alikiambia kituo cha redio cha Andalus, kinachowaunga mkono wapiganaji hao, kuwa hilo lilikuwa shambulio la kulipiza kisasi.

Al-Shabaab ilikuwa ikiidhibiti sehemu kubwa ya mji wa Mogadishu wakati wa miaka ya 2007 hadi 2011, lakini vikosi vya Umoja wa Afrika, vililifurumusha kundi hilo nje ya mji mkuu huo na miji mingine mikubwa. Marekani na Umoja wa Mataifa zimeonya kuwa mapigano ya kisiasa nchini Somalia yanaiweka hatarini hali ya usalama nchini humo.

Serikali ya shirikisho bado haina nguvu na ina uwezo mdogo sana nje ya mji mkuu, Mogadishu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE, AFPE, DPAE
Mhariri: Sekione Kitojo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi