Ugiriki: Kyriakos Mitsotakis ameapishwa
26 Juni 2023Waziri Mkuu wa Ugiriki, Mitsotakis alikula kiapo chake katika ikulu mbele ya kiongozi wa Kanisa la Kiorthodox la Ugiriki, kulingana na utamaduni wa kidini wa nchi hiyo. Rais wa Ugiriki Katerina Sakellaropoulou amempa Mitsotakis mamlaka rasmi ya kuendesha serikali. Kiongozi wa chama cha New Democracy, Kyriakos Mitsotakis alimtembelea Rais wa Ugiriki katika Ikulu mjini Athens leo Jumatatu asubuhi ili kupokea mamlaka ya kuunda serikali baada ya ushindi wake katika uchaguzi wa marudio mnamo siku ya Jumapili.
Amesema ni heshima kubwa kupokea majukumu hayo ya kuunda serikali kwa muda wa miaka minne. Kiongozi huyo wa chama cha New Democracy amekariri kuwa lengo lake tangu mwanzo lilikuwa ni kuunda serikali ya chama kimoja, huku akiahidi kwa mara nyingine tena kufanya mabadiliko makubwa na mageuzi ya kiuchumi nchini Ugiriki.
Mitsotakis anayekiongoza chama cha New Democracy amerejeshwa madarakani na idadi kubwa ya wapiga kura iliyowahi kushuhudia tangu karibu miaka 50 iliyopita kwenye chaguzi za nchini Ugiriki. Hayo ni kutokana na juhudi zake za kuleta utulivu wa kiuchumi hasa kwa kuzingatia mzigo wa madeni ya Umoja wa Ulaya.
Chama cha kihafidhina cha New Democracy kinachoongozwa na Kyriakos Mitsotakis kilipata asilimia 40.6 ya kura. Akiwa na viti 158 bungeni, waziri mkuu huyo sasa ana nafasi kamili ya kudhibiti wingi katika bunge lenye jumla ya viti 300. Mpinzani wake mkuu wa chama cha mrengo wa shoto cha Syriza, aliyekuwa zamani mkuu wa serikali, Alexis Tsipras, alipata asilimia 17.8.
Wagiriki wanasema wameshangazwa na wapiga kura walioamua kugeukia upande wa kulia lakini wanaafiki kwamba watu wa Ugiriki wana haki ya kufanya maamuzi bora yanayozingatia demokrasia na kwamba ni muda tu ndio utakaoonesha athari za kura hiyo.
Rais wa Marekani Joe Biden amesema anatarajia kuendelea kwa ushirikiano wa karibu katika vipaumbele vya pamoja ili kukuza ustawi na usalama wa kikanda. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia ameahidi ushirikiano kuelekea Ulaya yenye nguvu na uhuru zaidi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Antonio Tajani amesema kuchaguliwa tena kwa Mitsotakis ni ishara ya utulivu wa kisiasa ambayo ni nzuri kwa Ulaya nzima.
Vyanzo:DPA/AP/AFP/