Kiongozi wa Ghana aiomba radhi Nigeria
24 Juni 2020Kiongozi wa Ghana ameomba radhi kwa Nigeria kuhusiana na kuvunjwa kwa jengo la ubalozi wake mjini Accra, ofisi ya rais wa Nigeria imesema.
Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana jana alizungumza na rais Muhammadu Buhari wa Nigeria, ameeleza kuomba kwake radhi kutokana na kuvunjwa kwa jengo hilo katika eneo la ubalozi wa Nigeria mjini Accra, Ghana, imesema taarifa kutoka ofisi ya rais jana.
Akufo-Addo pia ameamuru uchunguzi kuhusu tukio hilo, taarifa imesema, na kuongeza kuwa baadhi ya washukiwa wamekamatwa na watashitakiwa.
Watu wenye silaha wanaripotiwa kuingia katika eneo la ubalozi huo wa Nigeria mjini Accra siku ya Ijumaa kuelekeza matrekta kuvunja jengo ambalo lilikuwa bado linajengwa. Waziri wa mambo ya kigeni wa Nigeria Geoffrey Onyeama siku ya Jumatatu alimuita balozi wa Ghana Iva Denoo mjini Abuja kudai kupata maelezo kuhusiana na tukio hilo.