1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Iran aondoa uwezekano wa mazungumzo na Marekani

Angela Mdungu
17 Septemba 2019

Kiongozi wa juu wa Iran Ali Khamenei, ameondoa uwezekano wa  mazungumzo na Marekani, huku maafisa wa Marekani wakidai kubadilishana taarifa na Saudi Arabia zinazoashiria Iran kuhusika na mashambulizi ya mwishoni mwa juma

Iran Teheran | Ayatollah Ali Khamenei spricht zu iranischen Geistlichen
Picha: picture-alliance/abaca/Parspix

Kauli ya Ali Khamenei, ya kuondoa uwezekano mazungumzo na Marekani imetolewa muda mfupi baada ya Rais Donald Trump kuilaumu Iran kuhusika na shambulizi la mwishoni mwa wiki dhidi ya  Saudi Arabia ambalo lililenga maeneo muhimu ya uzalishaji mafuta ya nchi hiyo na kusababisha kushuka kwa uzalishaji wa mafuta kwa asilimia tano duniani.

Ayatollah Ali Khamenei akitangaza msimamo wa nchi yake juu ya Mazungumzo na Marekani amesema iwapo Marekani itafuta kauli yake na kutubu baada ya kujiondoa katika mkataba wa Nyuklia wa Iran, hapo inaweza kujiunga na nchi nyingine ambazo bado zipo kwenye makubaliano na kisha itaweza kuzungumza na Iran sambamba na nchi hizo.

Hata hivyo, maafisa wa Marekani wamesema wanapanga kubadilishana taarifa zaidi kuhusu shambulio hilo na Saudi Arabia katika siku za hivi karibuni.

Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/J. Ernst

Trump amesema Marekani iko tayari kuisaidia Saudia lakini haitasubiri hadi hapo itakapothibitishwa rasmi kuwa ni nani hasa aliyehusika katika tukio hilo. Trump ameongeza kuwa, hana nia ya kuingia kwenye mgogoro mpya lakini wakati mwingine mtu hulazimika kufanya hivyo na kwamba shambulio dhidi ya Saudi Arabia lilikuwa kubwa.

Saudia, ambayo imekuwa ikiunga mkono vikwazo vya Marekani kwa Iran ilisema jana Jumatatu kuwa uchunguzi wa mwazo ulionesha kuwa silaha zilizotumika kushambulia miundombinu ya mafuta ni za Iran, ingawa haikuwa na ushahidi wa kuthibitisha hilo.

Kutokana na shambulio hilo, Iran imewaomba wataalamu wa kimataifa kujiunga na timu ya wachunguzi nchini humo ambao hadi sasa uchunguzi wao unaashiria kuwa shambulizi hilo halikufanywa kutokea Yemen kama ambavyo kundi la wahouthi lilivyotangaza. Wataalamu hao wamesema bado eneo ilipotokea ndege isiyo na rubani iliyohusika na shambulizi hilo halijabainika.

Mahusiano kati ya Marekani na Iran, yalizorota, baada ya Trump kujiondoa katika mkataba wa nyuklia wa Iran na kuiwekea vikwazo nchi hiyo. Trump anaitaka pia Iran kuacha kuyasaidia makundi kama lile la wahouthi  la Yemen ambalo limejitangaza kuhusika na shambulizi la Saudi Arabia la mwishoni mwa juma. Tukio la mwishoni mwa Juma nchini Saudi Arabia limezidisha mvutano na kuzua hali ya wasiwasi juu ya mgogoro huo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW