Kiongozi wa jeshi la Sudan amewasili Misri
29 Agosti 2023Mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan amewasili Misri katika safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu kuzuka kwa vita mwezi Aprili, huku ghasia za hivi karibuni zikisababisha vifo vya takriban watu 39 katika mkoa wa Darfur.
Burhan, amewasili katika mji wa pwani wa Misri wa El Alamein leo Jumanne ili kukutana na Rais Abdel Fattah al-Sisi. Hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa Burhan kuondoka Sudan tangu kuanza kwa mzozo kati ya jeshi la serikali na Kikosi cha msaada wa dharura RSF.
Misri ilijitolea kuwa mpatanishi kati ya pande zinazopigana za Sudan, katika mfululizo wa juhudi za kimataifa kuzuia kuendelea kwa muda mrefu vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuongezeka kwa mgogoro wa kibinadamu.
Soma pia: Burhan ajitokeza hadharani miezi 4 tangu vita vianze
Katika ziara hii, Burhan ameandamana na maafisa kadhaa akiwemo Waziri wa mambo ya nje Ali al-Sadiq, mkuu wa mamlaka ya ujasusi Jenerali Ahmed Ibrahim Mufadel, pamoja na maafisa wengine wa kijeshi.
Katika hotuba kwa wanajeshi kabla ya kuondoka Sudan, Burhan aliondoa matumaini ya kufanyika mazungumzo, akiishutumu RSF kwa kuwaita "wasaliti" na kuahidi ushindi wa uhakika.
Mauwaji Darfur
Huku haya yakijiri madaktari na mashahidi wamesema raia 39 wameuawa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, katika shambulio la makombora katika eneo la Nyala, mji wa pili wa Sudan katika jimbo la DarfurKusini ambako mapigano kati ya jeshi na wanamgambo yameongezeka.
Darfur kwa muda mrefu imekuwa eneo la mapigano makali tangu vita vilivyozuka mwaka wa 2003 ambapo kikosi cha Janjaweed, kilichozaa kundi la RSF walitekeleza ukatili dhidi ya makabila madogo.
Kuhusu hali ya kibinaadamu, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric hapo jana aliwambia waandishi wa habari kwamba Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu, UNFPA limewasilisha vifaa vya kutosha vya afya ya uzazi kusaidia wanawake na wasichana.
"Kutoka kwa wenzetu katika Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Darfur Magharibi, Mfuko wa Idadi ya Watu wa Umoja wa Mataifa umepeleka wafanyakazi wa afya na kijamii kusaidia maelfu ya wanawake na wasichana waliokimbia makazi yao na walio katika mazingira magumu na huduma za afya ya uzazi na ulinzi, ikiwa ni pamoja na kwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia. Na huko mashariki mwa Sudan jana, UNFPA iliwasilisha vifaa vya kutosha vya afya ya uzazi kusaidia wanawake na wasichana 150,000 kwa miezi mitatu katika Hospitali ya Wazazi ya Port Sudan."
Makadirio kutoka kwa mradi wa Armed Conflict Location & Event Data yanaonyesha kuwa karibu watu 5,000 wameuawa katika mzozo wa Sudan. Lakini takwimu halisi zinadhaniwa kuwa kubwa zaidi, na Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu milioni 4.6 wamekimbia makazi yao.