1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa juu Afghanistan awaonya wapiganaji kutovamia nje

6 Agosti 2023

Waziri wa ulinzi wa Afghanistan Mohammad Yaqoob Mujahid amesema kuwa kiongozi wa juu wa kidini Hibatullah Akhundzada amewaonya wanachama wa kundi la Taliban wasifanye mashambulizi nje ya nchi hiyo

Onyo hilo limetolewa siku chache baada ya Islamabad kudai kuwa raia wa Afghanistan walihusika katika mfululizo wa mashambulizi ya kujitoa muhanga Pakistan.

Katika hotuba yake iliyorushwa na televisheni ya taifa jana Jumamosi, Mujahid alieleza kuwa Hibatullah Akhundzada amesema kwamba ikiwa mtu yeyote atapigana nje ya nchi hiyo kwa madhumuni ya kupambania dini, mapambano hayo hayatoitwa Jihadi bali ni vita.

Tangu utawala waTaliban uliporejea madarakani miaka miwili iliyopita nchini Afghanistan, Pakistan imekuwa ikishuhudia wimbi la mashambulizi ya wanamgambo waliojikita zaidi katika maeneo ya mipaka upande wa magharibi. Kundi la Tehreek-e-Taliban Pakistan ambalo ni mshirika wa Taliban ya Afghanistan, na kundi hasimu linalojiita dola la Kiislamu IS, yote yamekiri kuhusika na mashambulizi hayo.