Hamas yaapa kuwazuia mateka hadi Israel itakapomaliza vita
18 Oktoba 2024Kwenye taarifa ya video iliyorekodiwa na kutangazwa na kituo cha televisheni cha Al Jazeera, kiongozi wa ngazi za juu wa kisiasa wa Hamas mwenye makao yake nchini Qatar, Khalil al-Hayya alisema na hapa namnukuu, "Tunamuomboleza kiongozi mkuu, kaka aliyeuawa kama shahidi, Yahya Sinwar, Abu Ibrahim,"
Akaongeza kuwa "Tunawaambia wale wanaowalilia wafungwa wa wavamizi, wanaoshikiliwa na Hamas kwamba, wafungwa hawa hawatarudi kwenu hadi pale Israel itakapokomesha uchokozi dhidi ya watu wetu huko Gaza, kujiondoa kikamilifu kutoka Gaza, na wafungwa wetu mashujaa waachiliwe kutoka kwenye magereza ya wavamizi."
Sinwar anadaiwa kuongoza shambulizi la Oktoba 7 mwaka uliopita nchini Israel, lililochochea vita kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza. Kulingana na Wizara ya Afya inayratibiwa na kundi hilo huko Gaza, hadi sasa vita hivyo vimesababisha vifo vya watu 42,500.
Na huko mjini Brussels, Marekani imeitolea wito Israel, Hamas na wanamgambo wa Hezbollah kutumia fursa ya kifo cha Sinwar kubadilisha hali ya mambo, hii ikiwa ni kulingana na Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin mapema leo.
Marekani na mataifa kadhaa mengine yanaamini Sinwar alikuwa kizingiti katika mchakato wa kufikia makubaliano ya usitishwaji wa mapigano.
Huko Tehran Iran, Waziri wa Mambo ya kigeni Abbas Araghchi ameandika kupitia ukurasa wa X kwamba kifo cha Sinwar kinaongeza tu msukumo kwa wanamgambo wanaopigana na Israel kote Mashariki ya Kati, iwe ni Wapalestina na ama sio Wapalestina kuliko ilivyowahi kushuhudiwa.
Wachambuzi wanaonya kwamba sintofahamu iliyosababishwa na kifo hiki cha Sinwar inaibua kitisho kikubwa. Mtaalamu wa Israel kuhusiana na masuala ya Hamas Guy Aviad anasema hivi sasa mateka watakabiliwa na hatari kubwa.
Amesema, inaaminika kwamba mdogo wa Sinwar ndiye aliyepewa jukumu la mustakabali wa mateka hao na kwa maana hiyo pengine atajaribu kulipiza kisasi.
Na huko Lebanon, kundi la wanamgambo la Hezbollah limesema ndio kwanza linaingia kwenye awamu mpya ya mapambano dhidi ya jeshi la Israel, hata baada ya sintofahamu iliyojitokeza sasa.
Katika hatua nyingine, Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema anaendelea kuunga mkono suluhu ya mataifa mawili kwenye mzozo huu, wakati akimwalika Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas kushiriki kwenye mkutano wa kilele wa kundi la BRICS huko Kazan, wiki ijayo, ambako suala hilo pia litajadiliwa.