Khamenei ataka Mlangobahari wa Hormuz uendelee kufungwa
12 Machi 2026
Katika hotuba hiyo, Khamenei amesema Iran inapaswa kuendelea kuufunga Mlango Bahari wa Hormuz na kuwa mashambulizi ya nchi yake katika mataifa ya Ghuba, yanapaswa kuendelea.
Katika hotuba yake iliyorushwa na Televisheni ya taifa ya Iran iliyosomwa na mtangazaji, Ayatollah Mojtaba Khamenei amesema kufungwa kwa mlango bahari wa Hormuz kunapaswa kutumiwa kama njia ya kutoa shinikizo zaidi dhidi ya Marekani na Israel.
Aidha ametoa wito kwa mataifa ya Ghuba kuzifunga kambi zote za kijeshi za Marekani la sivyo zitashambuliwa. Khamenei ameapa kulipa kisasi kwa ajili ya wote waliouwawa kwenye vita hivyo ikiwa ni pamoja na katika shambulizi lililoilenga shule. Ameahidi kuwa Iran italipwa fidia na adui na iwapo atakataa basi Iran itazichukua mali zake au kuziharibu kwa kiwango stahiki.
Iran imekuwa ikifanya mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara zinazopita kwenye mlango bahari wa Hormuz na miundombinu ya kibiashara tagu Marekani na Israel zilipoanzisha mashambulizi.
Licha ya mashambulizi hayo, Marekani kupitia Waziri wa Nishati Chris Wright imesema haiko tayari kuzisindikiza meli za mafuta zinazopita kwenye mlangobahari wa Hormuz ili kuzikinga na mashambulizi ya Iran.
Mashambulizi yanaendelea pande zote
Katika hatua nyingine, Iran imefanya awamu nyingine ya mashambulizi ya makombora dhidi ya Israel baada ya Israel kuishambulia Tehran usiku wa kuamkia Alhamisi. Jeshi la walinzi wa mapinduzi limesema lilirusha makombora pamoja na droni katika miundombinu ya kijeshi zikiwemo kambi za jeshi la anga za Palmachim na Ovda pamoja na makao makuu ya shirika la ndani la Ujasusi la Israel Shin Bet.
Nayo Israel imefanya mashambulizi mapya mjini Tehran ambayo wakaazi wake wameyaelezea kuwa ndiyo makali zaidi tangu vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vilipoanza.
Kwa mara ya kwanza, mashambulizi hayo yameripotiwa kuyalenga maeneo yenye watu wengi. Jeshi la anga la Israel limeripoti pia kuwa limeikishambulia kituo cha utafiti wa kijeshi cha Taleghan katika eneo la Parchin kusini mashariki mwa Tehran.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la kudhibiti nishati ya Atomiki, teknolojia zinazohusishwa na silaha za nyuklia zilikuwa zikitengenezwa kwenye kituo hicho kama sehemu ya mpango wa nyuklia wa Iran AMAD hadi kufikia mwaka 2003.
Wakati huohuo, Shirika la kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema karibu watu milioni 3.2 wamelazimika kuyahama makazi yao ndani ya Iran tangu vita vilipoanza. Mkuu wa huduma za dharura wa shirika hilo Ayaki Ito amesema kati ya kaya 600,000 hadi milioni moja zimeathiriwa na mzozo huo.