Pasaka: Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani ahimiza amani
9 Aprili 2023Matangazo
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ametoa ujumbe wa Pasaka katika uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Petro kwa kuhimiza uharaka wa kufuata njia za amani na udugu. Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki aliwaambia waumini wapatao 100,000 kwamba vita na mateso duniani vimegubika sherehe za Pasaka. Papa Francis ametoa wito wa kuishinda migogoro na migawanyiko na badala yake kufungua mioyo ya wanadamu kwa wale wanaohitaji zaidi. Katika siku hii muhimu, Papa Francis mwenye umri wa miaka 86 aliwakumbusha waumini juu ya vita vya Ukraine, ambapo aliitaka jumuiya ya kimataifa kufanya jitihada zote ili kukomesha vita hivi pamoja na migogoro yote inayochafua dunia kwa umwagaji damu yakiemo mataifa ya Lebanon, Haiti pamoja na Sudan Kusini.