1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Kanisa katoliki Papa Francis ziarani Japan

Oumilkheir Hamidou
23 Novemba 2019

Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni, Papa Francis amewasili Japan anakotarajiwa kutoa risala kali ya amani dhidi ya nuklea katika nchi pekee iliyowahi kuhujumiwa kwa mabomu ya atomiki.

Japan Papst in Tokio gelandet - unterwegs Gruß an Hongkong
Picha: AFP/B. Mehri

Kiongozi huyo wa kanisa katoliki ulimwenguni, mwenye umri wa miaka 82 anatekeleza dhamiri ya muda mrefu ya kuhubiri nchini Japan ambako miaka kadhaa iliyopita alitaraji angekuwa mmisionari.

Amewasili Tokyo na mvua kali na upepo, huku kofia yake nyeupe ikipeperushwa alipokuwa anateremka ngazi za ndege ya shirika la ndege la Thailand, akitokea Thailand.

Ziara yake ya siku nne itaanzia Nagasaki na Hiroshima, miji inayofungamanishwa daima na mabomu ya nuklea yaliyodondoshwa mwishoni mwa vita vikuu vya pili vya dunia na kuangamiza maisha ya watu wasiopungua 74.000 Nagasaki na 140.000 Hiroshima. Katika miji yote hiyo miwili Papa Francis atazungumza na wahanga wa mashambulio ya mabomu ya atomiki. Papa Francis atahutubia mbele ya kumbusho la amani mjini Hiroshima-ushahidi wa shambulio la bomu la nuklea lililodondoshwa  Agosti 6 mwaka 1945.

Watawa wakijiandaa kumpokea kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Papa FrancisPicha: AFP/E. Jones

Duwa ya kuiepushia dunia balaa la kudondoshwa mabomu ya nuklea

Katika ujumbe wake aliowatolea wananchi wa Japan kupitia kanda ya video kabla hajaondoka Vatican, Papa Francis alikosoa vikali "matumizi mabaya ya silaha za nuklea."

"Pamoja nanyi, naomba Mungu silaha za maangamizi za nuklea hazitotumika tena katika historia ya binadamu" amesema kiongozi huyo wa waumini bilioni moja nukta tatu wa kikristo ulimwenguni.

Papa Francis amewasili Tokyo akitokea Thailand ambako alihubiri uvumilivu wa kidini na amani. Anatarajiwa kutoa nasaha kama hiyo nchini Japan yenye waumini 440.000 tu wa kikatoliki kutoka jumla ya wakazi milioni 126.

Jumatatu Papa Francis atakutana na wahanga wa majanga ya kimaumbile, "matetemeko ya ardhi,Tsunami na kuvuja mionzi ya nuklea mwaka 2011" tukio lililoathiri sehemu kubwa ya kaskazini mashariki mwa Japan.

Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni amepangiwa pia kukutana na mfalme mpya Naruhito na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe pamoja na kuhutubia katika uwanja wa michezo mjini Tokyo.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Tatu Karema

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW