Kiongozi wa kijeshi Burkina Faso akubali kujiuzulu
3 Oktoba 2022Taarifa iliyotolewa Jumapili na viongozi wa kidini na wa kijamii imeeleza kuwa Luteni Kanali Damiba ameomba kujiuzulu jana ili kuepusha madhara yanayoweza kusababishwa na makabiliano dhidi ya raia na uharibifu wa mali. Hatua hiyo inatokana na mazungumzo yaliyofanyika kati ya Damiba na kiongozi mpya aliyejitangazia madaraka, Kapteni Ibrahim Traore.
Masharti ya kujiuzulu
Viongozi wa kidini waliosaidia katika juhudi za upatanishi wamesema Damiba ametoa masharti saba ili aweze kuondoka madarakani, ikiwemo kuhakikishiwa usalama na haki yake pamoja na usalama wa washirika wake katika jeshi. Pia amewataka waliochukua madaraka kuheshimu ahadi aliyoitoa kwa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS ya kurejesha utawala wa kiraia katika kipindi cha miaka miwili.
Kwa mujibu wa viongozi hao wenye ushawishi mkubwa nchini Burkina Faso, Traore, mwenye umri wa miaka 34 ameyakubali masharti yaliyowekwa na Damiba na amewaalika wananchi kuwa watulivu, kujizuia na ghasia na kusali.
Taarifa iliyotolewa jana na wanajeshi wanaomuunga mkono Traore imesema kuwa afisa huyo wa jeshi ataendelea kuwa kiongozi wa nchi hadi atakapoapishwa rais wa Burkina Faso aliyeteuliwa na vikosi vya jeshi la taifa hilo la Afrika Magharibi, katika tarehe ambayo haijatajwa.
Uungaji mkono mapambano dhidi ya wapiganaji wa jihadi
Traore ametangaza kuwa anaungwa mkono na makamanda wa kijeshi kuimarisha upya mapambano dhidi ya wapiganaji wa jihadi. Aidha, katika taarifa yake Jumapili, ECOWAS imepongeza hatua ya pande zote kukubali kukabidhi madaraka kwa njia ya amani na kuondoa tofauti zao. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ujumbe wa ECOWAS unatarajiwa kwenda Ouagadougou leo.
Baada ya kufanya mapinduzi, kiongozi huyo wa kijeshi amekutana na baraza la mawaziri na kusema kuwa nchi nzima iko katika hali ya tahadhari, na hivyo wanahitaji kuharakisha mambo. ''Kila mmoja katika hali hii anapaswa kufanya haraka na kuachana na urasimu na kufuata sheria. Burkina Faso kila kitu ni muhimu na cha haraka. Kuanzia usalama hadi ulinzi, afya, huduma za kijamii hadi miundombinu. Tunalazimika kusonga mbele haraka,'' alisisitiza Traore.
Wakati huo huo, duru za kidiplomasia za kikanda zimeeleza kuwa Damiba ambaye naye alichukua madaraka kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi mwezi Januari, 2022 Jumapili alikimbilia kwenye mji mkuu wa Togo, Lome.
Huku hayo yakijiri Ufaransa imelaani shambulizi lililofanywa na waandamanaji wenye hasira katika Ubalozi wa Ufaransa na majengo mengine nchini Burkina Faso. Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imekanusha madai ya uongozi mpya wa kijeshi kwamba Damiba alipewa hifadhi kwenye kambi ya kijeshi ya Ufaransa.
Mapinduzi ya Ijumaa yamekosolewa vikali na jumuia ya kimataifa ikiwemo Marekani, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na ECOWAS. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema Burkina Faso inahitaji amani, utulivu na umoja katika kupambana na makundi ya kigaidi na mitandao ya uhalifu inayoendesha shughuli zake kwenye maeneo ya nchi hiyo.
(AFP, AP, Reuters)