1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa kijeshi wa Mali amfuta kazi waziri mkuu

21 Novemba 2024

Kiongozi wa kijeshi wa Mali, Kanali Assimi Goita, amemuondoa waziri mkuu Choguel Maïga pamoja na serikali yake siku ya Jumatano, siku chache baada ya Maïga kuikosoa serikali ya kijeshi.

Kiongozi wa kijeshi wa Mali, Kanali Assimi Goita
Kiongozi wa kijeshi wa Mali, Kanali Assimi GoitaPicha: OUSMANE MAKAVELI/AFP/Getty Images

Kiongozi wa kijeshi wa Mali, Kanali Assimi Goita, amemuondoa waziri mkuu Choguel Maïga pamoja na serikali yake siku ya Jumatano, siku chache baada ya Maïga kuikosoa serikali ya kijeshi. Hatua hiyo ilitangazwa kupitia amri ya rais iliyosomwa na katibu mkuu wake kwenye kituo cha televisheni ya taifa, ORTM.

Mali imekuwa ikitawaliwa na viongozi wa kijeshi tangu mapinduzi ya mwaka 2020 na mapinduzi mengine mwaka uliofuata. Ingawa serikali ya kijeshi iliahidi kurejesha utawala wa kiraia kufikia Machi 2024, uchaguzi umesogezwa mbele bila tarehe maalum kutangazwa.

Maïga, aliyeteuliwa na jeshi miaka miwili iliyopita, aliilaumu serikali ya kijeshi kwa kuchelewesha uchaguzi bila kumjulisha na kuonya kuwa hali hiyo inaweza kuleta changamoto kubwa na kuhatarisha maendeleo. Baada ya matamshi hayo, utawala wa kijeshi uliandaa maandamano ya kumpinga Maïga. Mpaka sasa waziri mkuu mpya bado hajatangazwa.