1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Kiongozi wa kijeshi Myanmar aapa kuwaangamiza wanamgambo

27 Machi 2022

Utawala wa kijeshi Myanmar waapa kuwaangamiza wanamgambo wanaoendeleza harakati kubwa za kupinga mapinduzi ya kijeshi na utawala huo uliomuondowa madarakani kwa mabavu Aung San Suu Kyi

Myanmar Naypyitaw | Militärparade am Armed Forces Day
Picha: Aung Shine Oo/AP Photo/picture alliance

Kiongozi wa Myanmarameapa kuongeza hatua za kuyaandama makundi ya ndani ya wanamgambo yanayopambana dhidi ya serikali yake ya kijeshi akisema jeshi la nchi hiyo litawaangamiza wanamgambo  hao.

Min Aung Hlaing ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye gwaride la kuadhimisha siku ya vikosi vya kijeshi nchini humo ambapo pia ametowatolea mwito watu wa jamii za makabila ya waliowachache kutoyaunga mkono makundi hayo ya wanamgambo yanayoupinga utawala wa kijeshi na amekataa mazungumzo na makundi hayo.

Soma pia: Marekani yasema jeshi la Myanmar limefanya mauaji ya halaiki

Jeshi lilitwaa madaraka mwaka jana baada ya kumuondowa madarakani Aung San Suu Kyi ambaye serikali yake ilichaguliwa kidemokrasia nchini Myamar.

Hatua hiyo ya jeshi ilisababisha maandamano makubwa ya nchi nzima na kusababisha vifo vya zaidi ya raia 1,700 kwa mujibu wa takwimu iliyotolewa na taasisi inayotowa msaada kwa wafungwa wa kisiasa.

Jenerali Mkuu Min Aung Hlaing, mkuu wa baraza la kijeshi, akikagua gwaride la maafisa wakati wa amaadhimisho ya siku ya vikosi vya jeshi mjini Naypytaw, Myanmar, Jumapili, Machi 27, 2022.Picha: Aung Shine Oo/AP Photo/picture alliance

Wengi wa wanamgambo nchini humo wanaopambana na serikali ni watu waliokuwa wakiandamana kuipinga serikali ya kijeshi na waliolazimishwa kutoingia tena mitaani kuandamana kwa amani ambapo waliamua kuunda makundi ya wanamgambo yakijiita vikosi vya ulinzi wa wananchi, nchini humo vikijulikana zaidi kama PDF.

Katika baadhi ya maeneo ya Myanmar makundi hayo yamejiunga na makundi mengine ya vikosi vilivyojipanga vizuri vya kikabila  vyenye silaha ambavyo vimekuwa vikipambana kwa kipindi cha miongo kadhaa vikidai kudai uhuru mkubwa zaidi.

Soma pia: Umoja wa Ulaya umeiwekea vikwazo Myanmar

 Kiongozi wa serikali ya kijeshi ya Myanmar Aung Hlaing amesema hatokaa mezani kamwe na kile alichokiita makundi ya magaidi na wafuasi wao ambayo yanayouwa watu wasiokuwa na hatia na kutishia amani na usalama. Badala yake amesema jeshi la nchi yake linalojulikana kama Tatmadaw litawaandama mpaka litawamaliza wanamgambo wote hao.

Serikali yake imetangaza mapambano makubwa  dhidi ya makundi ya wanamgambo  bila ya kujali ikiwa makundi hayo yanajihusisha moja kwa moja katika mapambano ya silaha au makundi ya kigaidi.

Mafisa wa jeshi la Myanmar wakifanya gwaride kuadhimisha siku ya vikosi vya jeshi mjini Naypyitaw, Myanmar, Jumapili, Machi 27, 2022.Picha: Aung Shine Oo/AP Photo/picture alliance

Kwa mujibu wa utawala huo wa kijeshi kuna mwanachama au hata kuwa na mawasiliano na makundi hayo ni kitendo kinachobeba adhabu kali chini ya sheria.

Hlaing amesisitiza msimamo wake kwa kusema hakuna serikali yoyote au jeshi duniani ambalo linakaa chini na makundi yoyote ya magaidi kuzungumza. 

Soma pia: Jeshi Myanmar lampinga ujumbe wa ASEAN

Lakini licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa silaha na kikosi kikubwa jeshi la Myanamar limekuwa likipambana kuwaangamiza wanamgambo hao.

Vikosi vya wanamgambo wa PDF vimekuwa vikitegemea uungaji mkono wa jamii ndani ya nchi hiyo pamoja na uwezo mkubwa na maarifa ya kupambana ardhini kwenye msitu na mara nyingi hufanya mashambulizi ya kushtukiza yanayofanikiwa.

Ikumbukwe kwamba jeshi la Myanmar linatuhumiwa kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya jamii ya wachache ya warohingya na visa hivyo vimeorodheshwa na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa na mahakama ya kimataifa inatafakari kufungua mashataka ya mauaji ya halaiki dhidi ya jeshi hilo -Tatmadaw.

Chanzo: Mashirika