1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaGabon

Kiongozi wa kijeshi nchini Gabon asema hatakimbilia uchaguzi

2 Septemba 2023

Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Gabon yaliyomuondoa madarakani Rais Ali Bongo, jenerali Brice Oligui Nguema, amesema anataka kuepuka kukimbilia chaguzi zinazorudia makosa yaliopita.

Rais Ali Bongo aliyeondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi akipiga kura wakati wa uchaguzi mnamo Agosti 26, 2023
Rais Ali Bongo aliyeondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshiPicha: Gerauds Wilfried Obangome/REUTERS

Katika hotuba kupitia televisheni Ijumaa (1.09.2023) Nguema amesema kuwa uongozi wa kijeshi utaendelea kuchukuwa hatua za haraka lakini kwa umakini kuepeuka chaguzi zinazorudia makosa kwa kuwarudisha madarakani viongozi walioko kwa sasa.

Muungano wa vyama vya upinzani wataka utawala wa kiraia

Haya yanajiri wakati muungano wa vyama vya upinzani wa Gabon, umetoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kuhimiza viongozi waliompindua Rais Bongo, kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia. Msemaji wa muungano huo unaojulikana kama Alternance 2023, Alexandra Pangha, amelieleza shirika la habari la BBC kwamba wamefurahia kupinduliwa kwa Bongo, lakini wana matumaini kwamba viongozi wa mapinduzi watakabidhi mamlaka kwa utawala wa kiraia.

Soma pia:Gabon yasimamishwa uanachama katika Umoja wa Afrika

Wanajeshi wanambeba kiongozi wa mapinduzi jenerali Brice Oligui Nguema Picha: Handout/Gabon 24/AFP

Muungano huo unashinikiza kuhesabiwa upya kwa kura za uchaguzi wa Jumanne, ukikariri ushindi wa mgombea wa upinzani Albert Ondo Ossa.

Nguema asema taasisi za Gabon zitazingatia zaidi demokrasia 

Wakati huohuo, Nguema amesema kuwa taasisi za nchi hiyo zitazingatia demokrasia zaidi. Katika hotuba, Nguema amesema kuwa agizo la Jumatano la kuvunjwa kwa taasisi hizo ni la muda na kwamba ni suala la kuzipanga upya ili kuzifanya kuwa za kidemokrasia zaidi.

Soma pia:Viongozi wa Afrika kujibu hatua ya mapinduzi ya kijeshi Gabon

Nguema pia ameimarisha mawasiliano na makundi ya kitaifa na maslahi ya kigeni, na kukutana na wanachama wa mashirika ya kiraia siku moja baada ya hotuba kwa wafanyabiashara 200, ambao aliwasomea kuhusu rushwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW