1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Kiongozi wa kijeshi wa Sudan afanya ziara ya nne nje ya nchi

11 Septemba 2023

Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, anafanya ziara katika nchi jirani ya Eritrea. Hii ni safari yake ya nne nje ya nchi. Wakati huo huo, Shirika la Msalaba Mwekundu litapunguza bajeti yake kwa Sudan mwaka ujao.

Sudan | General Abdel Fattah Al-Burhan
Picha: Sudanese Army/AFP

Waziri wa Habari wa Eritrea, Yemane Meskel alitangaza kwenye mtandao wa kijamii wa X, kwamba Jenerali Burhan amewasili mjini Asmara Jumatatu, kwa ziara ya kikazi. Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ya Sudan, SUNA, mazungumzo kati ya Jenerali Burhan na Rais wa Eritrea, Isaias Afwerki, yatazingatia uhusiano wa nchi zao mbili, juu ya kuuimarisha uhusiano wao na migogoro ya nchini Sudan.

Kiongozi wa kijeshi wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah al Burhan.Picha: ASHRAF SHAZLY/AFP/Getty Images

Hii ni safari ya nne nje ya nchi ndani ya kipindi cha wiki mbili kwa Jenerali Abdel Fatah al-Burhan. Tangu Agosti 29 amezitembelea Misri, Sudan Kusini na wiki iliyopita, alikwenda nchini Qatar.

Soma:Kiongozi wa kijeshi wa Sudan akutana na kiongozi wa Qatar

Jenerali Abdel Fattah al Burhan amekuwa akitafuta uungwaji mkono wa kimataifa tangu mapigano kati ya jeshi la serikali analoliongoza na Kikosi Maalum cha Wanamgambo (RSF), kinachoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, yalipozuka na ambayo yameigeuza miji kadhaa kuanzia mji mkuu wa Sudan, Khartoum, na miji jirani ya Omdurman na Bahri, kuwa ni viwanja vya vita.

Wataalamu wanasema ziara ya kiongozi huyo wa Sudan ni sehemu ya juhudi za kujitengenezea sifa kimataifa endapo kutafanyika mazungumzo ya amani ya kumaliza vita nchi mwake.

Kwa miaka kadhaa, uhusiano kati ya Eritrea na Sudan umekuwa si mzuri. Sudan inawahifadhi wakimbizi wa Eritrea wapatao 126,000, wengi wao wakiwa ni wakimbizi waliokimbia mateso ya kisiasa na ukandamizaji kutoka nchini mwao Eritrea, kulingana na taarifa iliyochapishwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi.

Rais wa Eritrea, Isaias Afwerki.Picha: Khalil Senosi/AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo, makundi ya kikabila yenye ushawishi katika eneo la mashariki mwa Sudan ambayo yamekuwa yakifanya kampeni kwa muda mrefu ya kutaka kujitenga yamekuwa yakiungwa mkono na serikali ya Eritrea chini ya uongozi wa rais Isaias Afwerki.

Eritrea, ambayo inapakana na Sudan kwa upande wa kusini-mashariki, ni moja kati ya nchi jirani ambazo hazijapokea mkimbizi hata mmoja miongoni mwa zaidi ya wakimbizi milioni moja wanaokimbia vita nchini Sudan, kwa sababu mpaka huo umefungwa tangu mwaka 2019.

Mkurugenzi mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu, ICRC, Robert Mardini.Picha: Atta Kenare/AFP/Getty Images

Kwingineko, Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limetangaza kuwa litapunguza bajeti yake kwa Sudan ifikapo mwaka ujao kwa karibu asilimia 13. Mkurugenzi mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu, ICRC, Robert Mardini amesema hatua hiyo ni kutokana na wafadhili wakuu ikiwa ni pamoja na Marekani kupunguza ufadhili wao.

Soma:Umoja wa mataifa waomba msaada wa dola bilioni moja kuwasaidia wasudan

Mardini amesema kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu huku kukiwa na mizozo inayozidi kuongezeka duniani kote hali hiyo imelemea bajeti za misaada, na kuzilazimisha serikali ulimwenguni kote kufikiria upya maamuzi kuhusu nani wa kumsaidia na jinsi ya kutoa misaada hiyo.

Vyanzo: AFP/AP/RTRE

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW