1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa kimila Malawi aagiza ndoa za karantini zifutwe

Deo Kaji Makomba
27 Agosti 2020

Kiongozi mkuu wa kimila nchini Malawi amewaamuru machifu wa vijiji kufuta ndoa zote za watoto zilizofungwa wakati wa karantini ya covid-19 ili wasichana hao warudi darasani wakati shule zikitarajia kufunguliwa Septemba.

Nigeria Proteste gegen Kinderehe
Picha: picture alliance/AP Photo

Kiongozi huyo wa jadi , Chifu wa cheo cha juu, Theresa Kachindamoto, mwanaharakati maarufu dhidi ya ndoa za mapema, alisema kuongezeka kwa tabia hiyo haramu na vile vile mimba za mapema wakati wa janga hilo lilikuwa limemtia nguvu kushinikiza upya ili kuokoa ndoa za utotoni.

Kachindamoto alijiunga na juhudi za makundi ya wanawake ya kutetea haki za binadamu kwa ajili ya kueneza ujumbe wao miongoni mwa wazazi na viongozi wa vijiji katika maeneo yote ya taifa hilo la kusini mwa Afrika, ambako viwango vya juu vya ndoa za mapema vinaendelea licha ya marufuku ya 2015.

Soma pia Wavulana milioni 115 duniani kote waliingia ndoa za utotoni

Kachindamoto aliliambia shirika la wakiu wa Thomson Reuters kuwa "tumekuwa tukienda katika vijiji kushauri watu wawatunze watoto ili waweze kurudi shuleni wakati shule zitakapofunguliwa tena kwa sababu huko ndiko hatima ya maisha ya watoto hao iliko."

Chifu huyo pia alisema amewahi kuwaondoa baadhi ya machifu wengine wa jadi kwa sababu hiyo hiyo, kwa hivyo machifu wanafahamu fika kuhusu athari za kutofuata maagizo yake.

Wanafunzi wa shule ya sekondari mjini Lilongwe, Malawi.Picha: DW/M. Kaliza

Kwa upande wa wasichana ambao walipata ujauzito wakati wa kuwekwa vizuizi nchini Malawi ikiwemo kupiga marufu mikusanyiko ya watu na shule kufungwa kufuatia mlipuko wa virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa  COVID-19, Kachindamoto alisema alikuwa amewaambia machifu wa maeneo hayo wawahimize watoto warudi shuleni baada ya kujifungua.

Soma piaTatizo la mimba na ndoa za mapema

Sheria ya kupiga marufuku ndoa za utotoni

Malawi ilipitisha sheria ya kupiga marufuku ndoa za utotoni mnamo mwaka 2015 na kuongeza umri wa chini ambao msichana anaruhusiwa kuolewa kisheria hadi miaka 18, lakini bado matukio ya ndoa za utotoni yanaendelea kushamiri.

Karibu asilimia 47 ya wasichana nchini Malawi huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 na asilimia 9 wanakuwa bi harusi kabla ya siku ya kusherehekea umri wa 15, kulingana na shirika la watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF.

Soma piaBenki ya Dunia: Nchi zapoteza mabilioni ya mapato kwa ndoa za mapema 

Ndoa ya mapema sio tu inanyima wasichana fursa ya kupata haki ya elimu, lakini huongeza hatari ya kifo au majeraha makubwa wakati wa kujifungua kwa watoto ambao kimsingi miili yao bado haijakomaa.Mabibi harusi watoto pia wako katika hatari kubwa ya ukatili wa majumbani na ukatili wa kingono.

Ethiopia dhidi ya ndoa za utotoni

03:40

This browser does not support the video element.

Kuonyesha hali kama hiyo mahali pengine barani Afrika, maafisa na makundi ya misaada nchini Malawi wanasema wasichana wengi kuliko kawaida wamepata ujauzito au kuolewa wakati wa vikwazo vilivyowekwa kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona ambayo viliwalazimu watoto kutokwenda shule na kubakia majumbani na kusababisha shinikizo kwa vipato vya familia.

Mwanaharakati wa elimu Limbano Sapato alitoa mfano wa mji wa kusini wa Mangochi, ambapo visa vya mimba za wanarika na ndoa za utotoni ziliongezeka hadi 7,340 mnamo Julai mwaka 2020 kutoka 6,359 wakati wa mwezi kama huo huo mwaka jana.

Soma pia Unicef: Ndoa za utotoni zimepungua duniani

Maggie Kathewera Banda, mkurugenzi mtendaji wa shirika la haki za binadamu la Women's Legal Resource Centre, anasema haki za elimu za wasichana ziko hatarini.

Changamoto za wazazi kuhusu ada ya shule

Maafisa wa serikali waliunga mkono kampeni ya Kachindamoto na kuwasihi wazazi kuipa kipaumbele elimu ya watoto wao licha ya shida za sasa za kiuchumi zinazosababishwa na janga hilo la virusi vya Corona.

Waziri wa jinsia, Maendeleo na Ustawi wa jamii, Patricia Kaliati alisema baadhi ya wazazi wanapata wakati mgumu kuhakikisha wanapata ada ya shule kwa watoto.

Wanafunzi wa shule ya sekondari nchini Malawi.Picha: DW/M. Kaliza

Aidha waziri Kaliati alisema jamii zimejitolea kwa dhati na zimewashawishi kwamba wangependa kuwaelimisha watoto wao na amehihimiza watoto walioolewa waachwe warejee shuleni baada ya ndoa kuvunjwa kihalali.

Waziri huyo pia alisema mchakato wa kuzivunja ndoa hizo unapaswa, hata hivyo kulishirikisha kanisa na viongozi wengine wenye ushawishi katika jamii.

Soma pia Watoto milioni 700 wapokonywa utoto wao

Kulingana na shirika la misaada la Plan International na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, kufungwa kwa shule katika nchi 185 wakati wa COVID-19 kutaathiri vibaya wasichana waliobalahe kuongeza zaidi pengo la jinsia katika elimu na kusababisha kuongezeka hatari ya unyanyasaji wa kingono, mimba za mapema na ndoa za lazima.

Chanzo: Thomson Reuters Foundation