1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mikhail Gorbachev, kiongozi aliyemaliza vita baridi afariki

Sylvia Mwehozi
31 Agosti 2022

Kiongozi wa mwisho wa uliokuwa Umoja wa Kisovieti Mikhail Gorbachev, amefariki dunia akiwa na miaka 91. Viongozi wa ulimwengu wametuma salamu za pole wakimtaja kuwa na mchango mkubwa katika historia ya ulimwengu.

Michail Gorbatschow tot
Picha: Boris Yurchenko/AP/dpa/picture alliance

Gorbachev amefariki dunia jana katika hospitali mjini Moscow kutokana na maradhi ya muda mrefu. Mwanasiasa huyo ambaye alikuwa madarakani kati ya mwaka 1985 hadi 1991, alikuwa ndiye kiongozi wa mwisho wa enzi ya vita baridi.

Atakumbukwa kwa mchango wake wa kumaliza vita baridi bila umwagaji damu lakini akikosolewa kwa kushindwa kuzuia kusambaratika kwa Umoja wa kisovieti. Mnamo tarehe 25 Desemba mwaka 1991, Gorbachev aliyekuwa ameuongoza Umoja wa Kisovieti kwa miaka saba alijiuzulu wadhifa wake, na bendera ya muungano huo ilishushwa na kupandishwa ile shirikisho la Urusi. Kuanzia mwaka 1985 hadi kuanguka kwa muungano huo mwaka 1991, Gorbachev alisimamia mageuzi makubwa ya sera za kiuchumi na kisiasa za Urusi.

Rais wa Marekani Ronald Reagan(kushoto) na Mikhail Gorbatschow (kulia) mwaka 1986Picha: Ron Edmonds/AP Images/picture alliance

Alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1990 kwa kusaini mkataba wa kihistoria wa silaha za nyuklia na kiongozi wa Marekani wa wakati huo Ronald Reagan. Gorbachev alisema kuwa;

"Vizazi vijavyo vitatoa uamuzi wao juu ya umuhimu wa tukio ambalo tunakaribia kulishuhudia. Lakini nitathubutu kusema kwamba tunachofanya sasa, kusaini makubaliano ya kwanza kabisa ya kuondoa silaha za nyuklia, kuna umuhimu kwa ulimwengu wote binadamu, kutoka katika mtizamo wa siasa za ulimwengu na fikra za ubinadamu."

Mwanasiasa huyo aliungwa mkono katika mataifa ya magharibi kwa kuongoza mageuzi yaliyochochea uwazi na mjadala mkubwa wa umma ulioharakisha kuvunjika kwa himaya ya kisovieti. Hata hivyo nchini Urusi, kiongozi huyo aligubikwa na utata na kuwa na uhusiano mgumu na rais Vladimir Putin. Kwa Putin na Warusi wengi kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti, ilikuwa ni jambo la kusikitisha lililochangia muongo mmoja wa umaskini wa Urusi na kushuka kwa hadhi ya nchi hiyo katika uso wa dunia.

Gorbachev na Kansela mstaafu wa Ujerumani Angela Merkel mwaka 2011Picha: picture alliance/dpa

Viongozi wa ulimwengu wamkumbuka

Rais wa Urusi Vladimir Putin ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha kiongozi huyo. Salamu za pole pia zimetolewa na rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, aliyemuelezea kiongozi huyo kuwa "mtu mwenye mchango muhimu katika kumalizwa kwa vita baridi na aliyeondoa uhasama baina ya umoja wa kisovieti na nchi za magharibi, hatua iliyofungua njia ya "ulaya huru". Vita Baridi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika salamu zake za pole, amemsifu Gorbachev, kama "kiongozi wa kipekee aliyeibadilisha dunia kuwa bora". Amesema Gorbachev ni "mwanasiasa wa aina yake ambaye alibadilisha mkondo wa historia. Viongozi wengine waliotuma salamu za pole ni pamoja na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson wakimwelezea kuwa "mtu wa amani" aliyeonesha "uadilifu na ujasiri".

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW