1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Kiongozi wa RSF, Mohammed Daglo awekewa vikwazo

8 Januari 2025

Marekani imesema, vikosi vya (RSF) vimehusika na mauaji ya halaiki nchini Sudan na hivyo taifa hilo kubwa limemwekea vikwazo kiongozi wa kundi hilo la kijeshi Mohammad Hamdan Daglo

Sudan | Mohamed Hamdan Daglo
Picha: Ashraf Shazly/AFP

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema uamuzi huo umetokana na taarifa kuhusu mauaji ya "kudhamiria" yanayofanywa na vikosi vya RSF ambayo hasa yanawalenga wanaume na ubakaji kwa wanawake kutoka kwenye makabila fulani.

Blinken alipotangaza vikwazo dhidi ya Mohammad Hamdan Daglo kwa jukumu lake katika vitendo vya ukatili wa kimfumo unaofanywa dhidi ya raia amesema, Marekani imejitolea kuwawajibisha wote wanaohusika na dhulma hizo kwa watu wa Sudan.

Athari ya vita katika eneo la al-Fasher mji mkuu wa jimbo la Darfur, kaskazini mwa SudanPicha: AFP

Daglo anakabiliwa na lawama nzito kwa kuhusika kwake katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika jimbo la Darfur, ambako ripoti zinaeleza kwamba ubakaji mkubwa wa raia unafanywa na askari wa RSF chini ya udhibiti wake. Kiongozi huyo wa vikosi vya RSF pamoja na familia yake wamepigwa marufuku kuingia Marekani.

Soma Pia: Marekani yaishutumu Urusi kwa kufadhili vita Sudan 

Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari, uliopitishwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, unafafanua wazi kwamba mauaji ya halaiki ni "vitendo vinavyofanywa kwa nia ya kudhalilisha na kusambaratisha, kwa ujumla au kwa sehemu, taifa, kabila, watu kutokana na rangi yao au dini."

Tamko la Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani la kuviweka vikosi vya RSF na kiongozi wake kwenye orodha ya wanaohusika na "mauaji ya halaiki" ni la nadra likiwa ni kwa mara ya tisa kutolewa yakiwemo mauaji ya kimbari ya Wayahudi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kamanda mkuu wa RSF, Mohammad Hamdan Daglo, anawajibika kwa vitendo vya kuchukiza na vya haramu vinavyofanywa na vikosi vyake.

Wakati huo huo kampuni saba na raia mmoja wameunganishwa kwenye vikwazo hivyo vilivyowekwa na Marekani kwa kuhusika kwao katika kununua silaha kwa niaba ya vikosi vya RSF.

Kampuni hizo zinazomilikiwa na RSF katika Umoja wa Falme za Kiarabu ni pamoja na kampuni inayohusika na usafirishaji wa madini ya dhahabu ambayo yanadhaniwa kuwa huenda madini hayo husafirishwa nje ya Sudan kinyume cha sheria.

Raia wakimbia vita kutoka katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum wanaelekea Wad Madani mji ulio umbali wa kilomita 80 kutoka KhartoumPicha: AFP

Umoja wa Falme za Kiarabu, mshirika wa Marekani umekuwa akilaumiwa mara kwa mara kwa kuvipatia silaha vikosi vya RSF, lakini umekuwa ukikanusha vikali tuhuma hizo licha ya kuwepo ushahidi kwamba inahusika.

Soma Pia:  Sudan ipo katika hatari ya kukabiliwa na viwango vikubwa vya njaa

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Wally Adeyemo, amesema Marekani inaendelea kutoa wito wa kukomeshwa mgogoro wa Sudan ambao unaweka hatarini maisha ya raia wasio na hatia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema azimio la utawala Rais Joe Biden, halikusudii kuunga mkono upande wowote katika mzozo wa Sudan lakini badala yake linalenga kuongeza hatua za kuwawajibisha wanaohusika na uhalifu wa kivita na dhulma dhidi ya ubinadamu.

Vyanzo: AFP/AP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW