Kiongozi wa Scotland Sturgeon atangaza kujiuzulu
15 Februari 2023Kiongozi huyo wa chama kikubwa kabisa cha Scottish National - SNP amesema kuwa katika kichwa chake na moyoni mwake, anafahamu kuwa ni wakati mwafaka wa kuondoka, baada ya kukaribia muongo mmoja madarakani akishinikiza uhuru wa Scotland.
Sturgeon mwenye umri wa miaka 52 amethibitisha kuwa atasalia kuwa waziri kiongozi hadi pale chama cha SNP kitamchangua kiongozi mpya. Pia atabakia kuwa mjumbe wa Bunge la Scotland hadi angalau uchaguzi ujao, unoapangwa mwaka wa 2026.
Sturgeon anaondoka baada ya kukabiliwa na shinikizo kuhusu mbinu zake za uhuru na kuhusu haki za watu waliobadili jinsia. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Edinburgh, amesema, uamuzi huo hauhusiani kwa namna yoyote na masuala yaliyojitokeza hivi karibuni, bali anauchukua baada ya kujitathmini kwa muda mrefu.