1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Sudan akutana na ujumbe wa Nchi za Kiarabu

7 Novemba 2021

Mkuu wa Baraza la Kijeshi nchini Sudan Abdel Fattah al-Burhan, Jumapili amekutana na ujumbe wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu uliotumwa mjini Khartoum kutafuta suluhu ya mzozo unaoendelea nchini humo.

Putsch im Sudan | General Abdel Fattah al-Burhan
Picha: /AP/dpa/picture alliance

Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu ambayo imezitolea wito pande zinazozozana nchini Sudan kuendelea na kipindi cha mpito kuelekea demokrasia baada ya mapinduzi ya Oktoba 25, ilitangaza kuwa itatuma ujumbe wake mjini Khartoum siku ya Jumapili.

Ujumbe huo wa ngazi ya juu uko mjini humo katika wakati polisi ikipambana na waandamanaji wanaopinga mapinduzi ya kijeshi katika siku ya kwanza ya maandamano ya nchi nzima yaliyoitishwa kwa muda wa siku mbili kuanzia leo Jumapili.

Vikosi vya uslama vilifyetua mabomu ya machozi kuwatawanya walimu waliokuwa wakiandamana kupinga jeshi kuchukua hatamu za uongozi.

Makumi ya walimu walikusanyika nje ya wizara ya elimu mjini Khartoum wakiwa na mabango yaliyosomeka "hapana kwa utawala wa kijeshi" na kushinikiza kurejea kwa serikali ya mpito "chini ya viongozi wa kiraia."

Maandamano makubwa ya kupinga mapinduzi ya kijeshi ikiwemo yaliyohudhuriwa na mamia kwa maelfu ya watu mnamo Oktoba 30 yamefanyika tangu jeshi lilipotwaa madaraka mnamo Oktoba 25.

Waandamanaji mjini Khartoum wakiandamana dhidi ya jeshi la mapinduziPicha: Marwan Ali/AP/picture alliance

Hata hivyo yamekabiliwa na ukandamizaji mkubwa kutoka vyombo vya dola. Hadi sasa karibu waandamanaji 14 wameuwawa na wengine 300 kujeruhiwa.

Takwimu hizo ni kulingana na kamati huu ya madaktari wa Sudan.

"Tumeitisha maandamano ya amani na ya ukimya dhidi ya maamuzi ya Burhan nje ya wizara ya elimu " amesema Mohammed al-Amin, mwalimu wa Jiografia aliyeshiriki maandamano hayo ya siku ya Jumapili kumpinga Jenerali Abdel Fattah al-Burhan anayeongoza Baraza Tawala la Kijeshi nchini Sudan.

Idadi ndogo ya watu yajitokeza kwa maandamano ya Jumapili

Hata hivyo maandamano ya Jumapili hayakuwa makubwa kama yalivyotarajiwa kutokana na kukatwa kwa huduma ya mtandao na mawasiliano ya simu.

Picha: AFP

Wakaazi mjini Khartoum wanasema kuwa watu walijitokeza katika barabara za katikati mwa mji huo ijapokuwa kulikuwa na msongamano mdogo wa magari kuliko kawaida. 

Katika eneo la Kaskazini mwa Khartoum maafisa wa ulinzi walishika doria katika barabara kuu wakiwa wamebeba fimbo na mabomu ya kutoa machozi.

Baadhi ya wafanyakazi wa hospitali walifanya kazi kama kawaida wakati wengine wakishiriki kwenye mgomo.

Kamati za upinzani nchini humo pamoja na Muungano wa wazuoni wa Sudan SPA ulioongoza maandamano makubwa yaliyouangusha utawala wa muda mrefu wa rais  Omar al-Bashir mnamo mwaka 2019, zinapanga kampeni ya maandamano kujaribu kurejesha utawala wa kiraia nchini humo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW