1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

Kiongozi wa Syria asema serikali kudhibiti silaha zote

22 Desemba 2024

Kiongozi mpya wa Syria amesema silaha zote zitawekwa chini ya udhibiti wa serikali baada kuagushwa kwa utawala wa miongo kadhaa wa familia ya kina Assad.

Syria Damascus | Ahmad al-Sharaa
Kiongozi wa Syria Ahmed Al-SharaaPicha: Omar Albam/AP/dpa/picture alliance

Sharaa alieleza kuwa baada ya mashauriano yajayo na maafisa wa ulinzi na jeshi kuhusu muundo mpya wa kijeshi, vikundi vyenye silaha vitatangaza kuvunjika na kujiunga na jeshi.

Alisisitiza kuwa silaha zozote nje ya udhibiti wa serikali hazitaruhusiwa, iwe kutoka kwa vikundi vya mapinduzi au vile vilivyo katika eneo linalodhibitiwa na Kikosi cha Demokrasia cha Syria (SDF) kinachoongozwa na Wakurdi.

Soma pia: Kiongozi mpya Syria aahidi kuheshimu mamlaka ya Lebanon

Uturuki inaona sehemu kuu ya kikosi hicho kinachoungwa mkono na Marekani, ambacho kinadhibiti kaskazini na kaskazini-mashariki mwa Syria, kuwa na uhusiano na Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK), kilichopigwa marufuku nchini humo.

Sharaa alisema wanajitahidi kulinda madhehebu na jamii za wachache dhidi ya mashambulizi na wahusika wa nje wanaotafuta kuzua mfarakano wa kimadhehebu. Aliongeza kuwa, "Syria ni nchi ya wote na tunaweza kuishi pamoja kwa amani."

Kiongozi wa kundi la SDF Mazloum Abdi na Ahmed Al-Sharaa, Kiongozi mpya wa Syria.Picha: AFP/Omar Haj Kadour/AFP

Fidan: Trump anajua zaidi ya kuisaidia SDF

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, alisema Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, anaelewa umuhimu wa kuacha kuunga mkono wapiganaji wanaoongozwa na Wakurdi na badala yake kusaidia mahitaji ya kiusalama ya mshirika wake wa NATO, Uturuki.

Fidan pia alisisitiza kuwa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya utawala uliopita wa Syria vinapaswa kuondolewa haraka, akihimiza jamii ya kimataifa kushirikiana kuisaidia Syria kujikwamua na kuwezesha wakimbizi kurejea makwao.

Fidan alisema ushindi wa Syria ni matokeo ya juhudi za wananchi wake na kwamba Uturuki haina mkono katika mashambulizi yaliyomuondoa Assad madarakani. Alitaja ushindi huo kama nafasi ya kihistoria kwa Syria kufufua mshikamano wa kitaifa.

Aidha, Uturuki imekuwa ikipinga msaada wa Marekani kwa SDF, ambayo sehemu yake ni Kikundi cha Ulinzi wa Watu (YPG), ikikiona kama tawi la PKK. Marekani, hata hivyo, inakiona SDF kama mshirika muhimu katika kupambana na wanamgambo wa Dola ya Kiislamu (IS).

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan akisalimia na kiongozi mpya wa Syria Ahmed Al-Sharaa mjini Damascus, Desemba 22, 2024.Picha: Murat Gok/Anadolu/picture alliance

Marekani imeweka wanajeshi wake kaskazini mwa Syria kama sehemu ya muungano wa kimataifa dhidi ya IS, na Pentagon imeripoti ongezeko la wanajeshi wake hadi kufikia 2,000 mwaka huu. Washington inaamini uwepo wa SDF ni muhimu katika kuzuia kurudi kwa IS.

Soma pia: Watawala wapya Syria wateua waziri wao wa mambo ya nje

Uturuki inatarajia Trump kuchukua hatua ya kuondoa vikosi vya Marekani kutoka Syria, hatua aliyokuwa karibu kuchukua wakati wa muhula wake wa kwanza.

Fidan alionyesha matumaini kuwa Trump atashughulikia suala hilo kwa kipaumbele cha maslahi ya Marekani, akiongeza kuwa Uturuki inatarajia kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na Ankara kwa kuondoa msaada kwa SDF.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW