Kiongozi wa upinzani Msumbiji aitisha maandamano nchi nzima
12 Januari 2025Kiongozi wa upinzani wa Msumbiji Venancio Mondlane, ambaye alirejea nchini humo kutoka uhamishoni wiki iliyopita, ameitisha maandamano ya siku tatu wiki hii. Kurejea kwake nchini humo, kulichochea makabiliano kati ya wafuasi wake na polisi.
Katika ujumbe wake kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Mondlane ametoa wito wa maandamano ya nchi nzima, wakati bunge jipya likijiandaa kukutana siku ya Jumatatu.
Kiongozi huyo wa upinzani ameongeza kuwa siku tatu hizo za maandamano ni muhimu kwa watu wa Msumbiji ili kuamua mustakabali wanaoutaka. Amewahimiza wafuasi wake kufanya maandamano ya amani yatakayotatiza shughuli katika siku hizo tatu.
Rais Mteule kupitia chama tawala cha Frelimo Daniel Chapo anatarajiwa kusimikwa siku ya Jumatano. Mondlane anasisitiza kuwa aliibiwa ushindi katika uchaguzi uliopita wa mwezi Oktoba mwaka jana.