1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Myanmar : San Suu Kyi aongezewa muda wa kifungo cha nyumbani

Nijimbere, Gregoire27 Mei 2008

Viongozi wa kijeshi nchini Myanmar, wamemuongezea muda wa mwaka mmoja wa kifungo cha nyumbani kiongozi wa upinzani bi San Suu Kyi. Hatua hiyo ya viongozi wa kijeshi ni kama upuuzi wa mwito wa jamii ya kimataifa.

San Suu Kyi, kiongozi wa upinzani nchini MyanmarPicha: AP

Kelele za watu, hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa wakati wafuasi wa bi San Suu Kyi wakifanya maadamano karibu na nyumba yake wakiwataka viongozi wa kijeshi kumuachilia huru kiongozi wao.

Wito huo umepuuzwa kabisa na watawala wa kijeshi ambao badala ya kumuachia huru bi San Suu Kyi wameamua kumbakiza katika kifungo cha nyumbani kwa muda wa mwaka mwingine mmoja.

Afisa mmoja wa serikali ambae jina lake limehifadhiwa, amesema wajumbe wa serikali walifika nyumbani kwake bi San Suu Kyi kumuarifu juu ya hatua hiyo ambapo taarifa zilizochomoza zimezungumzia miezi 6 lakini mwanadiplomasia mmoja ambae pia hakutaka jina lake litajwe kathibitisha kwamba San Suu Kyi atafungwa mwaka mwingine mmoja. Polisi wamewakamata watu kiasi ya 20 mapema leo ambao wote ni wafuasi wa chama cha San Suu Kyi cha kitaifa kwa ajili ya demokrasi, NLD.


Mbali na wafuasi wake, hatua hiyo ya kumuoongezea muda wa kifungo cha nyumbani bi San Suu Kyi, umetafsiriwa pia kama kuwavunja moyo wafadhili ambao walikuwa wameahidi kuitolea misaada mingi ya kifedha Myanmar kwa sharti la kumuachia huru mwanasiasa huyo, nchi hiyo ya Myanmar ikihitaji misaada wakati huu hasa baada ya kukumbwa na kimbunga kikali kwa jina Nargis mapema mwezi huu, ambacho kilisababisha watu zaidi ya 130.000 kuuliwa au kutoweka na wengine kiasi ya milioni 2 na laki 4 kuyapoteza maskani yao na kuhitaji misaada ya dharura.


Watetezi wa haki za binaadamu wamemkosoa vikali Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon ambae kwa maoni yao, hakuthubutu hata kulitaja jina la San Suu Kyi alipokuwa ziarani nchini Myanmar hivi karibuni kuzungumza na viongozi wa nchi hiyo juu ya mbinu za kurahisisha utoaji misaada ya dharura kwa wahanga wa kimbunga. Kulingana na Mark Farmaner wa kituo cha kufuatilia hali ya mambo nchini Myanmar kilichoko Uingereza, Bwana Ki Moon amekwepa kutamka ukweli asiwakasirishe viongozi wa nchi ambao hadi sasa hawajaregeza kamba ili kuruhusu wanaoleta misaada wote kwa wahanga wa kimbunga waweze kuitoa bila tatizo.

Bi San Suu Kyi alikamatwa tena tarehe 30 Mei mwaka 2003 baada ya shambulio la msafara wa magari yake karibu na mji wa kaskazini wa Depayin ambapo watu wanne waliuawa katika mapigano kati ya wafuasi wake na wale wa serikali.


Chama cha San Suu Kyi kiliibuka mshindi katika uchaguzi wa bunge miaka 18 iliopita lakini kikanyimwa nafasi ya kuitawala nchi na kiongozi wake kuanza kukabiliwa na kifungo cha nyumbani. Kwa muda huo basi wa miaka 18, San Suu Kyi, ameshazuwiliwa nyumbani miaka 12 kijumla.




Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW