1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bobi Wine aruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kujeruhiwa

4 Septemba 2024

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine aliruhusiwa kutoka hospitalini Jumatano baada ya kufanyiwa upasuaji wa jeraha la mguu alilolipata wakati wa makabiliano na polisi. Polisi imemlaumu WIne kwa kukadi miongozo.

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda na rapa Bobi Wine
Kiongozi wa chama cha NUP, Bobi Wine katika moja ya harakati zake za kisiasa.Picha: Ronald Kabuubi/AP/picture alliance

Awali, Chama cha Bobi Wine cha National Unity Platform, NUP, kilisema mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 42, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Sentamu, alipigwa risasi mguuni na polisi na kueleza kuwa ni "jaribio jingine la kumuua kiongozi huyo wa chama."

Lakini NUP baadaye ilisema Wine alipigwa na bomu la machozi na alipelekwa hospitalini mjini Kampala. "Alifanyiwa upasuaji ambapo vipande vya bomu la kutoa machozi vilitolewa kwenye mguu wake na ametengemaa na yuko njiani kutoka hospitali sasa," meya wa Kampala Erias Lukwago aliiambia AFP.

Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha Wine, akiwa amevikwa blanketi ya rangi ya maziwa na bandeji mguuni, akisukumwa kwenye kiti cha magurudumu na wafanyikazi wa hospitali.

Wine na chama chake cha NUP kwa muda mrefu wamekuwa mwiba kwa Museveni, ambaye ameitawala Uganda kwa mkono wa chuma kwa takriban miaka 40.

Soma pia: Bobi Wine kupasuliwa baada ya kujeruhiwa mguuni

Nyota huyo wa zamani wa pop, ambaye alichuana na kiongozi huyo mkongwe katika uchaguzi wa 2021, amewekwa kizuizini au kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani mara nyingi na mikutano ya chama chake imetawanywa kwa vurugu.

Bobi Wine amekuwa akikabiliana nguvu kubwa ya polisi tangu alipojiunga na siasa na kuonyesha kuwa tishio kwa mkongwe Yoweri Museveni.Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

"Inaonekana polisi walilenga kumdhuru," wakili wake George Musisi aliambia AFP kuhusu tukio la Jumanne.

Musisi alisema Bobi Wine alijeruhiwa wakati polisi walipofyatua mabomu ya machozi hovyo dhidi ya kundi dogo la wafuasi mjini Bulindo, alikokuwa ameenda kuhudhuria mkutano wa kisiasa.

"Bomu la machozi lilifyatulia dhidi yake kulipukia na mguuni,” alisema na kuongeza kuwa polisi pia wamewakamata wafuasi wanne wa chama hicho.

 Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zilimuonyesha Bobi Wine akiugulia maumivu.

Polisi yachunguza na kudai WIne alijijeruhi mwenyewe

Maafisa wa polisi wa Uganda walisema wanachunguza tukio hilo, huku msemaji Kituuma Rusoke akisema maafisa watatu pia walijeruhiwa katika vurugu hizo.

"Wacha tusubiri wataalamu wafanye kazi yao na kuchunguza," Rusoke aliuambia mkutano na waandishi wa habari Jumatano. "Tuna changamoto, hata hivyo, na wanasiasa ambao hawaheshimu mwongozo wetu hasa kwenye maandamano kwenye barabara kuu," alisema.

"Kwa sababu hiyo Kyagulanyi alijeruhiwa, maafisa watatu wa polisi walijeruhiwa na magari ya polisi yalishambuliwa," alisema.

Adui wa Museveni ni Museveni mwenyewe - Bobi Wine

06:34

This browser does not support the video element.

Soma pia: Polisi Uganda yazuwia mapokezi ya Bobi Wine

Taarifa ya polisi ya Uganda iliyotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumanne ilisema maafisa katika eneo la tukio walipingana na maelezo ya upinzani, wakisema Bobi Wine alijikwaa na kujijeruhi wakati akiingia kwenye gari lake.

Ilisema Wine na timu yake walikuwa wameanza maandamano kinyume na ushauri wa polisi.

Baada ya tukio la Jumanne, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Matthew Miller alisema Washington ina wasiwasi kwamba "nafasi  ya demokrasia inaendelea kupungua" nchini Uganda.

Mwezi Julai, polisi walikandamiza maandamano ya kupinga ufisadi mjini Kampala, wakiwakamata na kuwashtaki makumi ya waandamanaji, na pia wamekamata watu waliokuwa wanaandamana kupinga mradi mkubwa wa mafuta katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki mara kadhaa.

Uganda itapiga kura Januari 2026, miaka mitano baada ya mkongwe Museveni kuchaguliwa tena kwa muhula wa sita. Upinzani ulilaani kura ya 2021 ulioitaja kuwa ya udanganyifu, kufuatia kampeni iliyoambatana na vitisho, kukamatwa kwa upinzani na ghasia.

Chanzo: AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW