Kiongozi wa upinzani Urusi, Navalny, arejeshwa jela
29 Julai 2019Mwakilishi wa hospitali ameliambia shirika la habari la Urusi TASS kwamba Navalny tayari ameshapatiwa matibabu na amerejeshwa jela.
Awali leo hii, daktari wa Navalny, Anastasiya Vasilyeva, amesema sumu huenda ikawa imemsababishia kuugua na anapinga hatua ya kurejeshwa jela mwanasiasa huyo.
Navalny alipelekwa hospitali Jumapili kutoka jela ambako anatumikia kifungo cha siku 30 kwa kuitishwa maandamano yaliyokatazwa na serikali. Alikamatwa siku chache kabla ya kufanyika maandamano makubwa ya upinzani Jumamosi iliyopita, ambayo yalipelekea watu 1,400 kutiwa mbaroni na polisi.
Vasilyeva, ambaye ni daktari wa Navalny kwa miaka kadhaa, amesema leo kuwa alimkuta mwanasiasa huyo akiwa amevimba uso pamoja na kujawa na vipele hali inayoashiria kuwa alipewa sumu.
"Ninawasihi wenzangu wamuweke chini ya uangalizi wa kimatibabu kwa angalau siku tatu, hadi uchunguzi wa kitafiti utakapokuwa tayari. Lakini, nasikitishwa na amri iliyotolewa kutoka juu. Sasa hivi ameongozwa na polisi hadi chumba cha ulinzi," amesema Vasilyeva.
Elena Sibikina, mmoja wa madaktari waliomtibu Navalny amewaambia waandishi habari kwamba madai ya kuwa amepewa sumu hayakuweza kuthibitishwa. Daktari huyo ameongeza kwamba maisha ya Navalny hayapo hatarini.
Ujerumani yataka waandamanaji waachiliwe huru
Navalny amekuwa akiikosoa serikali ya Urusi tangu mwaka 2011, alipoongoza maandamano makubwa ya kumpinga Rais Vladimir Putin na chama chake tawala.
Tangu wakati huo ameshakutikana na hatia kwa mshtaka ya aina mbili tofauti, na amekuwa akishikiliwa jela mara kwa mara kwa kuvuruga utulivu wa umma na kuongoza maandamano yaliyopigwa marufuku na serikali.
Ujerumani leo imeitolea wito serikali ya Urusi, haraka kuwaachilia huru watu 1,400 waliokamatwa wakati wa maandamano makubwa ya mjini Moscow yaliyofanyika mwishoni mwa juma. Maripota wa shirika la habari la AFP wameshuhudia waandamanaji kadhaa waliopata majeraha, kutokana na polisi kutumia marungu wakijaribu kuwatawanya.
Ulrike Demmer, msemaji wa kansela wa Ujerumani Angela Merkel, pia ameisisitizaUrusi kuheshimu uhuru wa kujieleza na kuandamana na kuhakikisha viwango vya kimataifa vinazingatiwa wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Septemba.