1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani Venezuela ajitangaza kuwa rais wa mpito

Sylvia Mwehozi
24 Januari 2019

Kiongozi wa upinzani wa Venezuela Juan Guaido amejitangaza kuwa rais wa kipindi cha mpito akiungwa mkono na Marekani pamoja na mataifa kadhaa ya Amerika ya Kusini. Maduro amevunja uhusiano wa Kidiplomasia na Marekani. 

Venezuela Juan Guaido, vorläufiger Präsident in Caracas
Picha: Getty Images/AFP/F. Parra

Rais wa Marekani Donald Trump amemtambua rasmi Guaido muda mfupi baada ya tangazo lake na kusifu mipango yake ya kuitisha uchaguzi. Canada nayo pia imeunga mkono hatua hiyo. Katika mkutano wa hadhara mjini Caracas mbele ya maelfu ya wafuasi wake, Guaido alimtuhumu Maduro kwa kujitwalia madaraka na kuahidi kuunda serikali ya mpito itakayolisaidia taifa hilo kuvuka kipindi kigumu cha anguko la uchumi.

Tangazo hilo la Guaido linauzidisha mzozo unaoiukumba Venezuela, kukiwa na uwezekano wa upinzani sasa kuendesha serikali inayotambuliwa na mataifa ya kigeni kama kiongozi halali lakini akikosa udhibiti wa shughuli za kitaifa. Kwenye hotuba yake kwa njia ya televisheni katika ikulu ya rais, Maduro amelaani upinzani kwa jaribio la mapinduzi linaloungwa mkono na Marekani na kumtuhumu kiongozi wa upinzani kwamba anatafuta kuendesha serikali kutoka mjini Washington.

"Mbele ya mwenyezi Mungu, Venezuela na kwa heshima ya wenzangu wote ndani ya bunge la taifa, ninaapa kuchukua madaraka ya urais kulitumikia taifa la Venezuela," alisema Guaido.

Rais Maduro akiwahutubia wafuasi wake katika ikulu ya rais Picha: Reuters/Miraflores Palace

Waziri wa ulinzi wa Venezuela Vladmir Padrino amesema jeshi halimtambui kiongozi huyo wa upinzani na linatoa hakikisho la uhuru wa kitaifa. Nchi 11 kutoka kundi la Lima la nchi za Amerika ya Kusini, lililoundwa mwaka 2017 kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Venezuela, nazo zimemuunga mkono Guaido. Hata hivyo Mexico, Saint Lucia na Guyana ambazo ni wanachama wa kundi hilo hazikutia saini zikisema zinafuatilia hali nchini Venezuela.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema Umoja wa Ulaya utatoa taarifa siku ya Alhamis kuhusiana na vita vya madaraka huko Venezuela. Hata hivyo mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo, Federica Mogherini awali alisema sauti za watu wa Venezuela haziwezi kupuuzwa na kutoa wito wa kufanyika uchuguzi huru na wa haki. Maduro amewapatia masaa 72 wanadiplomasia wa Marekani kuondoka nchini humo baada ya kuvunja mahusiano ya kidiplomasia na Marekani.

"Nimeamua kuvunja uhusiano wa kidplomasia na serikali ya Marekani. Waondoke ndani ya Venezuela, imetosha! Hatutaki kuingiliwa tena. Tuna utu hapa na kuna watu wa kuitetea nchi hii," alisema Maduro.

Urusi imesema hatua za kumshinikiza Maduro kuondoka madarakani si halali, huku Uturuki pia ikumuunga mkono Rais Maduro. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amempigia simu Maduro kumhakikishia kuwa wanamuunga mkono na kumhimiza kusimama kidete.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kuwepo majadiliano Venezuela ili kuepusha mzozo wa kisiasa kuwa mbaya zaidi na kusababisha kile alichokitaja janga kwa raia wa Venezuela na kuiathiri kanda nzima.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/reuters/dpa/afp

Mhariri: Caro Robi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW