1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UtamaduniKimataifa

María Machado ashinda Tuzo ya Amani ya Nobel

10 Oktoba 2025

Mwanaharakati wa upinzani wa Venezuela María Corina Machado ameshinda Tuzo ya Amani ya Nobel 2025 kwa ujasiri wa kupigania demokrasia na uchaguzi huru licha ya vitisho. Kamati ya Nobel imemsifu kwa kuunganisha upinzani.

Venezuela Caracas 2025 | Kiongozi wa upinzani María Corina Machado katika maandamano kabla ya kuapishwa kwa Maduro.
Kiongozi wa upinzani wa Venezuela, María Corina Machado, akiwahutubia wafuasi wake wakati wa maandamano kabla ya kuapishwa kwa Rais Nicolás Maduro kwa muhula wake wa tatu, mjini Caracas, Venezuela, Januari 9, 2025.Picha: Leonardo Fernandez Viloria/REUTERS

Mwanaharakati wa upinzani wa Venezuela, María Corina Machado, ametangazwa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya 2025, kwa mchango wake mkubwa katika kupigania demokrasia, haki za binadamu, na umoja wa kisiasa katika taifa lake lililokumbwa na mgogoro wa muda mrefu.

Tangazo hilo lilitolewa Ijumaa mjini Oslo, Norway, na Joergen Watne Frydnes, Mwenyekiti wa Kamati ya Nobel, aliyesema Machado “amekuwa kiungo muhimu cha umoja katika upinzani uliokuwa umepasuka – akisaidia kuunganisha wanasiasa na raia chini ya madai ya uchaguzi huru na utawala wa kidemokrasia.”

Frydnes aliongeza kuwa: “Katika mwaka uliopita, Bi. Machado amelazimika kuishi mafichoni. Licha ya vitisho vikali dhidi ya maisha yake, amebaki nchini Venezuela, jambo lililowatia moyo mamilioni. Wakati watawala wa kiimla wanaposhika madaraka, ni muhimu kuwatambua watetezi jasiri wa uhuru wanaosimama na kupinga.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Nobel ya Norway, Jørgen Watne Frydnes, akiwahutubia waandishi wa habari wakati akitangaza mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya 2025 katika Taasisi ya Nobel ya Norway, mjini Oslo, Norway, Oktoba 10, 2025.Picha: Rodrigo Freitas/NTB/AFP/Getty Images

Machado, aliyewahi kugombea urais kabla ya kuzuiwa na serikali ya Nicolás Maduro, amekuwa nembo ya upinzani wa amani. Amejipatia heshima kwa kukataa kuondoka nchini licha ya vitisho, kifungo cha nyumbani, na mashinikizo makubwa ya kisiasa.

Anajulikana kwa jitihada zake kupitia harakati ya Súmate, iliyohamasisha uwazi wa uchaguzi na ushiriki wa wananchi katika siasa za kidemokrasia. Ushindi huu wa Nobel unamfanya kuwa Mvenezuela wa kwanza kutunukiwa Tuzo ya Amani.

Trump alitarajiwa — lakini hakupata

Kabla ya tangazo hilo, kulikuwa na tetesi kwamba tuzo hiyo ingeenda kwa Rais wa Marekani Donald Trump, kufuatia juhudi zake za kusitisha vita vya Gaza. Hata hivyo, wachambuzi walionya kuwa hatua hizo zilikuwa za hivi karibuni mno na haziwezi kufikia vigezo vya Nobel vinavyozingatia matokeo ya muda mrefu ya amani na ushirikiano wa kimataifa.

Wataalamu wanasema Kamati ya Nobel kwa kawaida huzingatia “uendelevu wa amani, udugu wa kimataifa na juhudi kimyakimya za taasisi zinazolinda misingi hiyo.”

Waandamanaji wakibeba mabango yenye picha za Rais wa Marekani Donald Trump na maandishi “Nobel.”Picha: Ammar Awad/REUTERS

Tangazo la leo linaendeleza urithi wa Alfred Nobel, aliyesisitiza tuzo hiyo itolewe kwa wale wanaochangia kuimarisha udugu kati ya mataifa na kupunguza migogoro. Frydnes alisema tuzo ya Machado ni “ushindi wa ujasiri dhidi ya hofu.”

Mwaka jana, tuzo hiyo ilienda kwa Nihon Hidankyo, harakati ya waathirika wa mabomu ya nyuklia kutoka Japan, waliopigania marufuku ya matumizi ya silaha hizo.

Sauti kutoka Caracas

Baada ya tangazo, wafuasi wa Machado walijitokeza mitaani mjini Caracas kushangilia. Kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), Machado aliandika:
“Tuzo hii ni ya watu wa Venezuela. Ni ushindi wa amani, uthubutu na matumaini.”

Rais Donald Trump alimpongeza kupitia taarifa fupi, akisema: “Huu ni ushindi wa demokrasia juu ya udikteta.” Wakati huo huo, viongozi wa Ulaya na Amerika Kusini walimpongeza Machado kwa “uongozi wa kishujaa katika enzi ya giza la kisiasa.”

María Corina Machado akipeperusha bendera ya taifa katika mkutano wa hadhara mjini Caracas, Agosti 28, 2024.Picha: Pedro Rances Mattey/AFP/Getty Images

Tuzo ya Amani ya Nobel ndiyo pekee inayotolewa Oslo, Norway, huku nyingine — tiba, fizikia, kemia, fasihi na uchumi — zikitolewa Stockholm, Sweden. Mchakato wa uteuzi huanza Januari kila mwaka na unahusisha majadiliano ya miezi kadhaa.

Kila mshindi hupokea medali ya dhahabu ya karati 18, cheti cha heshima, na zawadi ya fedha ya takriban dola milioni 1.2 za Marekani. Sherehe rasmi ya utoaji tuzo itafanyika Desemba 10, kumbukumbu ya kifo cha Alfred Nobel.

Chanzo: RTRE, APE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW