1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa waasi asema mkataba wa Marekani na DRC ni batili

29 Januari 2026

Kiongozi wa muungano wa waasi wa AFC/M23 nchini DRC, Corneille Nangaa, amesema mkataba wa kimkakati wa madini kati ya Kinshasa na Washington una kasoro kubwa za kisheria, mwaka mmoja baada ya waasi wa M23 kuiteka Goma.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Goma 2025 | Uongozi wa M23 katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa mapigano.
Kiongozi wa vuguvugu la AFC-M23 Corneille Nangaa (katikati) anasema Marekani iliasaini makubaliano ya kimkakati na upande usio sahihi.Picha: Cyrile Ndegeya/Anadolu/picture alliance

Kiongozi wa muungano wa waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), unaojumuisha kundi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, amesema mkataba wa madini kati ya Kinshasa na Washington una kasoro kubwa na hauzingatii katiba, hali inayotia shaka utekelezaji wake.

Corneille Nangaa, anayeliongoza kundi la Alliance Fleuve Congo (AFC), alikuwa akizungumzia makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati yaliyosainiwa Washington tarehe 4 Desemba, ambapo Marekani inatarajiwa kupata fursa kubwa ya kuchimba madini muhimu ya DRC kwa kubadilishana na uwekezaji na ushirikiano wa kiusalama.

Akizungumza na shirika la habari la Reuters mjini Goma Jumatatu, Nangaa alisema mpango huo unaathiriwa na ukosefu wa uwazi na kasoro za kisheria, akitaja kile alichokiita "usiri unaozunguka mazungumzo” na "makosa ya kiutaratibu, hususan ukiukaji wa Katiba na sheria.”

Ukosoaji wa Nangaa unaibua maswali zaidi kuhusu uwezekano wa utekelezaji wa uwekezaji wa Marekani mashariki mwa Congo, eneo lililokumbwa na vita, mwaka mmoja baada ya waasi wa M23 kuiteka Goma, mji mkubwa zaidi wa eneo hilo, kupitia mashambulizi ya kushtukiza.

Rais wa Marekani Donald Trump, Rais wa Rwanda Paul Kagame (katikati) na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi (kulia) baada ya kusaini makubaliano ya amani Desemba 04, 2025 mjini Washington, DC.Picha: Chip Somodevilla/Getty Images/AFP

Ofisi ya rais yauita wasiwasi kuhusu mktaba kuwa 'uvumi'

Sehemu kubwa ya madini muhimu ya mashariki mwa Congo, yakiwemo coltan, yako katika maeneo yanayodhibitiwa sasa na M23, ambayo imechukua maeneo makubwa ya uchimbaji kama Rubaya katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Nangaa alisema maeneo ya migodi yanayopendekezwa kupewa Washington huenda yakazua migogoro baadaye kwa sababu tayari yanaweza kuwa yamekabidhiwa washirika wengine.

"Wamarekani huenda wamesaini mkataba huo, lakini wanapaswa kujua kuwa wamesaini na utawala usio halali, na tena uliojaa rushwa,” alisema.

Ikijibu madai hayo, ofisi ya rais wa DRC iliyapinga vikali, ikisema ushirikiano huo "uko kikamilifu ndani ya mamlaka ya kikatiba” ya rais aliyechaguliwa na serikali.

Ilisema hofu kuhusu migogoro ya baadaye na waliopo tayari kwenye mikataba ni "ya kubashiri tu,” na kusisitiza kuwa ushirikiano wowote utaheshimu mikataba halali na kufuata sheria za uchimbaji madini za Congo.

Serikali ya Congo imesema mkataba huo utawasilishwa bungeni kwa ajili ya kuidhinishwa mwezi Machi. "Tuna wingi wa wabunge wanaotuunga mkono, hivyo tunaamini tutapata idhini ya bunge,” alisema Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchumi wa Taifa, Daniel Mukoko Samba, akizungumza na Reuters mjini Davos wiki iliyopita.

Waasi wa AFC-M23 wanadhibiti mikoa ya Kivu ambayo ina utajiri mkubwa wa madini inayokodolea macho Marekani.Picha: AFP

Uhusiano na Rwanda

Katika mahojiano hayo na Reuters, Nangaa alisema AFC inafanya kazi na majirani Rwanda na Uganda katika masuala ya kiusalama, lakini alikanusha kupokea msaada kutoka Kigali.

Rwanda inakanusha kuiunga mkono M23, ingawa ripoti ya jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa Julai ilieleza kuwa Kigali ilikuwa na ushawishi wa moja kwa moja wa uongozi na udhibiti juu ya waasi hao.

Wiki iliyopita, balozi wa Rwanda nchini Marekani alisema katika taarifa kuwa Kigali inashiriki katika "uratibu wa kiusalama” na AFC/M23.

Kutwaliwa kwa Goma, mji wenye zaidi ya wakazi milioni mbili ulioko mpakani mwa Congo na Rwanda, kuliashiria mojawapo ya milipuko mikubwa zaidi ya mapigano katika miaka ya hivi karibuni mashariki mwa Congo.

Nangaa alisema usalama umeimarika katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa waasi tangu walipochukua mji huo, akiongeza kuwa shule na hospitali zinafanya kazi kawaida na watu waliokuwa wamekimbia makazi yao wamerudi.

Hata hivyo, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema M23, majeshi ya serikali ya Kongo na makundi mengine yenye silaha yamefanya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, baadhi yake ukifikia kiwango cha uhalifu wa kivita. Pande zote zinakanusha madai hayo.

Rwanda yakiri kushirikiana na waasi wa M23

01:13

This browser does not support the video element.

Nangaa aliishutumu serikali ya Kinshasa kwa kuzuia juhudi za amani, akisema makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyojadiliwa Doha kwa usuluhishi wa Qatar na kuungwa mkono na Marekani hayajatekelezwa.

Serikali ya Congo imekanusha madai hayo, ikiwalaumu waasi kwa kuendelea kwa ghasia.

Mwezi Desemba, vikosi vya M23 viliingia kwa muda mfupi katika mji wa Uvira, vikisema vilitaka kuzuia mashambulizi dhidi ya raia, kabla ya kuondoka tena.

Nangaa alionya kuwa hatua zaidi haziwezi kuondolewa endapo hali ya ukosefu wa usalama itaendelea.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW