Kiongozi wa waasi wa Libya akutana na Waziri Mkuu wa Uingereza
12 Mei 2011Wakati huohuo, waasi wanaripotiwa kushangilia baada ya kuwafurusha kutoka mji wa Misrata wanajeshi wanaomtii kiongozi wa Libya. Kwa upande mwengine, kiongozi wa baraza la waasi kwa mara ya kwanza amefanya kikao cha ana kwa ana na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron. Azma yao ni kuujadili uwezekano wa kufungua afisi mjini London na pia utekelezaji wa yaliyoafikiwa kwenye kikao cha Roma wiki iliyopita.
Gaddafi bado yu hai
Kituo cha televisheni ya taifa kilizionyesha kanda za Kanali Muammar Gaddafi akiwa mkutanoni na maafisa wa serikali katika hoteli moja mjini Tripoli. Hatua hiyo imeziondoa tetesi zilizokuwa zimesambaa kuwa hatima yake haijulikani hasa baada ya mwanawe kuuawa katika shambulio la NATO la mwishoni mwa mwezi Aprili.
Kwa upande wake Jumuiya ya Kujihami ya NATO inashikilia kuwa shabaha ya operesheni inayoiongoza Libya si kuwadhuru raia wa kawaida. Claudio Gabellini ni mkuu wa operesheni za NATO anasisitiza kuwa:
"NATO kamwe haikusudii kumlenga mtu binafsi. Dhamira yetu ni kuusambaratisha mfumo unaozisimamia operesheni zinazowawezesha wanajeshi wa Kanali Gaddafi kuwashambulia raia pindi wanapoamriwa, jambo linaloyahatarisha maisha kadhalika kuikwamisha shughuli ya kuingiza misaada nchini humo."
Gwanda la hudhurungi na kofia nyeusi
Kiongozi huyo wa Libya alionekana akiwa amevaliwa gwanda lake maarufu la hudhurungi, miwani na kofia nyeusi. Kanali Muammar Gaddafi alikuwa hajaonekana na umma tangu ndege za NATO ziushambulie uwanja wake, kitendo kilichowaua mwanawe wa mwisho na wajukuuze watatu. Ukanda huo uliorushwa kwenye kituo cha televisheni cha Al Jamahiriya ulikuwa na tarehe ya jana Jumatano.
Kwa mujibu wa waandishi wa habari waliokuwako kwenye hoteli hiyo, wageni walipigwa marufuku kusogea karibu na baadhi ya vyumba vilivyokuwa vimetengwa mahsusi kwa matumizi ya Kanali Muammar Gaddafi.
Wakati huohuo, hapo jana jioni, waasi wa Libya wanaripotiwa kuwa waliuteka uwanja wa ndege ulioko mjini Misrata baada ya mapambano makali. Kulingana na waasi hao, huo ulikuwa ushindi mkubwa na walisisitiza kuwa wamefanikiwa kuzikamata silaha nyingi za aina tofauti.
Hata hivyo hakuna aliyezithibitisha taarifa hizo za ushindi. Ifahamike kuwa mji wa Misrata unaodhibitiwa na vikosi vinavyomtii Kanali Muammar Gaddafi kwa kipindi cha wiki nane sasa, una umuhimu mkubwa kwasababu una bandari na azma ya waasi ni kuuteka nyara. Kwa sasa waasi wa Libya wanaudhibiti mji wa Benghazi ulioko eneo la Mashariki kuliko na viwanda muhimu vya mafuta.
Hali ni mbaya
Kwa upande mwengine, mashirika ya kutetea haki za binadamu na misaada yanatahadharisha kuwa hali ya maisha inazidi kuwa mbaya. Takwimu zinaeleza kuwa kiasi ya watu nusu milioni wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na dawa. Hapo jana Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alitoa wito wa kusitisha mapigano haraka iwezekanavyo, "Mosi, lazima mapigano yakome mjini Misrata na kwengineko. Baada ya hilo ndipo tutakapoweza kuendelea kutoa misaada inayohitajika pamoja na kuupa msukumo mchakato mzima wa kisiasa," alisisitiza.
Kwa mujibu wa msemaji wa waasi hao aliyezungumza kwa simu akiwa kwenye milima ya Zintan, waasi hao wanakatakata kuuitikia wito huo na wakasisitiza kuwa muda wa kuchukua hatua hiyo umekwisha na hawamuamini Kanali Gaddafi. Operesheni ya Odyssey New Dawn nchini Libya ilianza tarehe 19 mwezi wa Machi na NATO kuchukua usukani wa kuiongoza mwishoni mwa mwezi huohuo.
Mwandishi: Mwadzaya, thelma-AFPE/RTRE, NATO-UN Multimedia
Mhariri: Yusuf, Saumu Ramadhan