1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Kundi la Wagner lasema limeingia Urusi bila pingamizi

24 Juni 2023

Kiongozi wa kundi la mamluki wa Urusi la Wagner Yevegeny Prigozhin, amesema Jumamosi (24.06.2023) kuwa wapiganaji wake wamevuka mpaka kutoka Ukraine kuingia Urusi bila kukabiliana na upinzani wowote.

Wagner Gruppe Yevgeny Prigozhin / Jewgeni Wiktorowitsch Prigoschin
Picha: Lev Borodin/TASS/dpa/picture alliance

 

Prigozhin amesema kambi za kundi hilo la Wagner zilishambuliwa kwa roketi na mizinga kwa amri kutoka kwa mkuu wa Utumishi wa Jeshi Valery Gerasimov. Prigozhin anadai kuwa Gerasimov alitoa agizo hilo baada ya mkutano na Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu, ambapo waliamua kuliangamiza kundi hilo la wagner

Kundi la Wagner liko mjini Rostov nchini Urusi

Ameongeza kuwa wapiganaji wa Waganer walikaribishwa na walinzi wa mpakani huku wakisogea katika eneo la Rostov na sasa wanaelekea katika mji wa Rostov. Prigozhin amesema maafisa waliokuwa katika maeneo ya ukaguzi wa usalama hawakutoa upinzani wowote na kuongeza kuwa vikosi vyake havipigani na ''watoto''. ''Tutakabiliana na yeyote atakayetoa upinzani, tunasonga mbele na tutaendelea hadi tamati'' ameongeza Prigozhin.

Prigozhin atoa wito wa uasi wa kijeshi

Mapema siku ya Ijumaa, Prigozhin alitoa wito wa uasi wa kijeshi unaolenga kumuondoa waziri wa ulinzi wa Urusi. Vyombo vya usalama vikajibu mara moja kwa kuanzisha uchunguzi wa jinai dhidi ya Prigozhin na kutoa wito wa kukamatwa kwake.

Sergei Shoigu - Waziri wa ulinzi wa UrusiPicha: Russian Defence Ministry via REUTERS

Prigozhin alichapisha mfululizo wa video na rekodi za sauti ambapo alimshtumu Shoigu kwa kuagiza shambulizi hilo dhidi ya kambi za Wagner nchini Ukraine ambapo wapiganaji wake walikuwa wanapigana kwa niaba ya Urusi.

Prigozhin alihimiza jeshi kutotoa upinzani wa aina yoyote

Prigozhin amelihimiza jeshi la nchi hiyo kutotoa upinzani na kutangaza kuwa hayo sio mapinduzi ya kijeshi bali maandamano ya haki. Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Ugaidi, ambayo ni sehemu ya huduma za usalama za serikali hiyo ya shirikisho ama FSB, imesema Prigozhin atachunguzwa kwa tuhuma ya kuitisha uasi wa kijeshi.

FSB yawahimiza wapiganaji wa wagner kutofuata maagizo ya Prigozhin

FSB imewahimiza wapiganaji wa kundi la wagner kumkamata Prigozhin na kukataa kufuata maagizo yake ya uhalifu na amri za usaliti. FSB ilitaja matamshi ya Prigozhin kuwa usaliti kwa vikosi vya Urusi na kusema ni sawa na kuzusha mzozo wa kivita nchini Urusi.