Sudan yamuita nyumbani balozi wake wa Kenya
5 Januari 2024Kwenye taarifa iliyorushwa na shirika rasmi la habari la SUNA, kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Ali al-Sadiq amesema balozi huyo amerejeshwa nyumbani kwa mashauriano ya kupinga mapokezi rasmi yaliyoandaliwa na serikali ya Kenya kwa ajili ya kiongozi huyo wa wanamgambo.
Amesema mashauriano hayo yataangazia uwezekano wa namna hatua hiyo inavyoweza kuathiri uhusiano kati ya Kenya na Sudan.
Dagalo, ambaye vikosi vyake vinapambana na jeshi la Sudan linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan amekua ziarani katika baadhi ya mataifa ya Afrika ambayo ni pamoja na Uganda, Ethiopia na Djibouti, Kenya na sasa yuko Afrika Kusini.
Uhusiano baina ya Burhan na serikali ya Kenya umekuwa katika mvutano kwa miezi kadhaa, wakati Nairobi ikiangazia kuendeleza mawasiliano na Daglo ili kusuluhisha mzozo baina ya majeshi hayo mawili ya Sudan.
Soma pia: Vikosi vya RSF nchini Sudan vimefanikiwa kuingia Wad Madani
Katika hotuba yake ya Januari 1, Jenerali Burhan alionya kwamba serikali za Afrika zinazoandaa ziara za "wauaji hao" "zinajionyesha dhahir kuwa ni washirika katika mauaji ya watu wa Sudan".
Juhudi za upatanishi kwa kiasi kikubwa zimesimama katikati ya ongezeko la uadui kati ya majenerali hao wawili.
Vita hivyo vimesabaisha vifo vya zaidi ya watu 12,000, hii ikiwa ni kulingana na makisio ya taasisi ya Armed Conlfict Location and Dat Event Project, huku zaidi ya watu milioni 7 wakilazimika kuyakimbia makazi yao, umesema Umoja wa Mataifa.