Kipi chanzo cha mzozo wa Pakistan na Afghanistan?
30 Julai 2010Wasiwasi umezuka kuwa tukio hilo la hati kuvuja huenda likayahatarisha maisha ya raia wa kawaida.Yote hayo yanajitokeza wakati ambapo Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amekamilisha ziara yake siku mbili iliyompeleka India.Katika ziara yake ya kwanza ya Asia,kiongozi huyo pamoja na mwenyeji wake India wameitolea wito Pakistan kupambana na wapiganaji wa kundi la Taleban.Jee,kipi chanzo cha mzozo wa Afghanistan na Pakistan?
Wakazi milioni 22
Eneo la kaskazini magharibi mwa Pakistan lina kiasi cha wakazi milioni 22 wengi wao wa kabila la Pashtun.Inaaminika kuwa maeneo hayo ndiyo maficho ya viongozi wakuu wa mtandao wa kigaidi,Mullah Omar na Osama bin Laden.Wapiganaji wa kundi la Taleban wameyaimarisha mashambulio yao wanayoyaendesha kutokea eneo hilo la Pakistan.Harakati za wapiganaji hao zinauathiri mchakato mzima wa kutafuta amani Afghanistan na pia kutisha kuuvuruga uongozi wa Pakistan.Pakistan na Afghanistan zimekuwa zikilaumiana kwasababu ya hali ya usalama katika eneo hilo.Rahimullah Samandar,mchambuzi wa masuala ya uhusiano kati ya Afghanistan na Pakistan na mwandishi anaamini kuwa,''
Uhusiano kati ya Afghanistan na Pakistan unatatizwa na kutoaminiana.Mazungumzo rasmi ya ushirikiano yamekuwa yakiendelea ila hali halisi inaonyesha kuwa harakati hizo hazipo,''jambo linalochangia katika hali jumla ya usalama.
Tatizo hilo lilianza wakati wa ukoloni wakati mipaka ya eneo hilo ilipochorwa na Uingereza.Kwa upande wake Afghanistan ilikataa katakata kuitambua mipaka hiyo na ikadai kuwa azma ya hatua hiyo ni kuliteka eneo la waPashtun.Kufuatia hilo,wakazi hao wa Kipashtun waliamua kupambana na Pakistan ili kulinyakua eneo lao.Chini ya uongozi wa Zia-ul-Haq,madrassa nyingi zilijengwa katika eneo hilo ili kuyaendeleza maadili ya utawala wa Kiislamu.
Ni katika madrassa hizo,vijana walifunzwa itikadi kali.Mmoja wa vijana hao ni Osama bin Laden.
Mwanya wa mashambulio
Uingereza iliutumia mwanya huo wa kushambuliana kuichokoza Urusi,kuivuruga Pakistan iliyoiona kuwa kitisho na kwa upande mwengine kuimaliza nguvu serikali ya Afghanistan yenyewe.Pakistan ilizibadili mbinu zake na kuanza kuwatumia vijana waliosoma kwenye madrassa waliojazwa itikadi kali badala ya viongozi wa kitamaduni.Makundi ya Mujahideen ya Afghanistan yaliamua kujisimamia yenyewe ili kuivutia Pakistan.Hata hivyo yalizongwa na mivutano ya ndani na baada ya hapo kundi la Taleban lilizinduliwa na likachukua hatamu ya uongozi wa Afghanistan.Pakistan na Saudi Arabia pekee ndizo zilizoutambua utawala wa Taleban.
Kufuatia shambulio la mabomu la tarehe 11 mwezi wa Septemba mwaka 2001,Marekani iliamua kuivamia Afghanistan kwa lengo la kupambana na wapiganaji wa Taleban na magaidi wa Al-Qaeda.Kulingana na Sayfuddin Sayhun,mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mhadhiri ,njia ya kufuata ni moja tu ya,''Kupata suluhu ya kisiasa.Wakazi wa eneo hilo wanahitaji suluhu ya kudumu itakayowawezesha kuwa na miradi ya maendeleo,elimu na kuishi maisha ya kawaida kwa jumla.Bila ya hayo hakuna amani yoyote itakayopatikana,''alieleza.
Kauli hizo zimeungwa mkono na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron aliyeihitimisha Alhamisi usiku ziara yake ya India.Katika tamko lao la pamoja,viongozi wa India na Uingereza wameitolea wito Pakistan kupambana na uasi katika eneo hilo unaozivuruga harakati za kutafuta amani.
Mwandishi:Thelma Mwadzaya-ZPR-Shamel Ratbil
Mhariri:Josephat Charo