Kipimo kwa timu za Afrika kwenye mashindano kombe la Dunia
1 Julai 2026
Usiku wa leo ni wa maamuzi kwa soka la Afrika katika Kombe la Dunia 2026. Baada ya Afrika Kusini na Côte d'Ivoire kuyaaga mashindano, matumaini ya bara sasa yapo mikononi mwa DR Kongo na Senegal, ambazo zinakabiliwa na vigogo wa Ulaya, England na Ubelgiji. Je, Afrika itaandika historia nyingine?
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itakuwa na kibarua kizito dhidi ya England, timu inayotajwa kuwa miongoni mwa wanaowania ubingwa. Lakini kwa mashabiki wa Kongo, mechi za mtoano zina sheria zake; jina kubwa pekee halitoshi kushinda. "Uingereza na vipaji vyake vyote vile wana Kombe moja tu la Dunia, yaani hawatuzidi sana,"alisema shabiki Christian Kimahenga
Kocha wa DR Kongo, Sébastien Desabre, amesema kikosi chake kinaiheshimu England, lakini hakitasita kupambana kwa nguvu zote kutafuta ushindi. Kocha huyo amesema mchi hiyo itakuwa ngumu na tushikilia kuwa,timu ya taifa pia ina uwezo mkubwa."Tutapigania bendera ya Kongo kwa mbinu na nguvu zetu. Katika mechi ya mtoano, chochote kinaweza kutokea",alisema kocha huyo.
Hata nchini Uingereza, baadhi ya wachambuzi wameonya kuwa DR Kongo inaweza kuwa mtego kutokana na safu yake imara ya ulinzi na mashambulizi ya kushtukiza.
Wakati huo huo, macho ya Waafrika yatahamia kwenye pambano lingine kati ya Senegal na Ubelgiji. Simba wa Teranga wanaamini bado wana nafasi ya kuendelea na safari yao.
Kocha wa timu hiyo Pape Thiaw amesema kikosi chake kipo tayari kabisa kwa mpambano wa leo."Tunataka kuendelea mbele na kufikia malengo yetu., lakini nasi tuna kikosi chenye uwezo wa kushindana na timu yoyote,"alisema meneja huyo.
Mchambuzi wa soka Ramazani Kahambwe anaamini DR Kongo inaweza kuisumbua England ikiwa itadumisha nidhamu, huku akiipa Senegal nafasi halisi ya kuiondoa Ubelgiji.
Usiku wa leo unaweza kuwa wa furaha au majonzi kwa soka la Afrika. Je, DRC itaandika ukurasa mpya dhidi ya England? Je, Senegal itaivusha Afrika hatua ya 16 bora?