1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Kipindupindu chaua 172 Sudan, wagonjwa ni zaidi ya 2,500

29 Mei 2025

Sudan anazidi kutikiswa na mlipuko wa kipindupindu ambacho kimeua mamia na kuwauguza maelfu wengine katikati mwa mporomoko wa huduma za afya uliosababishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Sudan | Patienten mit akuter Diarrhöe | Archivbild 2017
Picha: Central Committee of Sudanese Doctors/AP Photo//picture alliance

Wimbi jipya la kipindupindu limeikumba Sudan, likiwa tayari limewaua watu 172 huku zaidi ya 2,500 wakiugua katika kipindi cha wiki moja tu.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, visa vya ugonjwa huo vimeongezeka kwa kasi, hususan katika miji ya Khartoum na Omdurman, ambako watu wengi waliokuwa wakikimbia vita wameanza kurejea, wakikuta miundombinu ya afya na usafi ikiwa imeporomoka kabisa.

Taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF) ilisema visa vya maambukizi viliongezeka kutoka wastani wa wagonjwa 90 kwa siku hadi 815 kati ya Mei 15 na 25. Kwa ujumla, zaidi ya watu 7,700 wamethibitishwa kuugua kipindupindu tangu mwanzo wa mwaka huu, wakiwemo zaidi ya watoto 1,000 walio chini ya umri wa miaka minne.

Hali ni mbaya zaidi katika vituo vya matibabu vinavyoendeshwa na Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka mjini Omdurman. Joyce Bakker, mratibu wa shirika hilo Sudan, alisema: "Wagonjwa wengi wanawasili wakiwa tayari wamechelewa kuokolewa. Hatujui kiwango kamili cha mlipuko huu, lakini hali tunayoshuhudia ni ya kusikitisha sana.”

Sababu za mlipuko wa kipindupindu

Chanzo kikuu cha maambukizi kimehusishwa na upatikanaji wa maji machafu, hususan katika maeneo ya Khartoum na Omdurman ambayo yalikuwa uwanja wa mapigano makali kati ya jeshi la serikali na kundi la Rapid Support Forces (RSF). Ingawa maeneo hayo yalichukuliwa tena na jeshi Machi, watu takribani 34,000 waliorejea hukumbana na mazingira machafu, ukosefu wa umeme na maji safi, huku mifumo ya usafi ikiwa imeharibiwa vibaya.

Watu wakisubiri huduma katika mmoja ya vituo vinavyotoa huduma za afya Sudan. Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Dr. Rania Elsayegh kutoka shirika la Sudan Doctors for Human Rights alisema: "Watu wanakunywa maji yaliyotapakaa uchafu na kuyahifadhi kwenye vyombo visivyo safi, hali inayochochea maambukizi.” Kwa upande mwingine, zaidi ya asilimia 80 ya hospitali nchini humo hazifanyi kazi tena, na zilizobaki zinakabiliwa na uhaba wa dawa, umeme na maji.

Kipindupindu ni nini?

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kipindupindu ni ugonjwa wa kuharisha unaosababishwa na bakteria aina ya "Vibrio cholerae", unaoenea kupitia chakula au maji machafu. Ingawa unatibika kwa urahisi kupitia maji ya kurejesha maji mwilini na dawa, unaweza kuua ndani ya saa chache kama haujatibiwa mapema. WHO imeeleza kuwa akiba ya chanjo ya kipindupindu imepungua duniani kote, wakati ambapo milipuko inaongezeka kutokana na umasikini, migogoro na mabadiliko ya tabianchi.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza Aprili 2023 kati ya jeshi la serikali na RSF vimesababisha vifo vya watu zaidi ya 24,000, huku zaidi ya milioni 14 wakifungasha virago, wakiwemo zaidi ya milioni 4 waliokimbilia nchi jirani. Ukame, mafuriko ya kila mwaka, na njaa katika maeneo kama Darfur vimeongeza mateso.

Vita hivyo pia vimehusisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa halaiki na mauaji ya kikabila ambayo Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu yameyataja kuwa uhalifu wa kivita na dhidi ya ubinadamu.

Vita vya Sudan vimeharibu sehemu kubwa ya mji mkuu KhartoumPicha: Ebrahim Hamid/AFP/Getty Images

Historia ya milipuko mingine

Sudan imekumbwa na milipuko ya kipindupindu mara kadhaa hapo awali. Mwaka 2017, watu zaidi ya 700 walifariki na wengine 22,000 waliugua katika kipindi cha chini ya miezi miwili.

Mwezi Septemba na Oktoba mwaka jana, kipindupindu kilienea katika majimbo 11 kati ya 18, na kusababisha vifo vya watu 626.

Mnamo Februari na Machi mwaka huu, mlipuko mwingine uliua watu 90 na kuwaathiri zaidi ya 2,600, wengi wao wakiwa katika jimbo la White Nile.

Mbali na kipindupindu, Sudan pia imekumbwa na magonjwa mengine ya milipuko. Wiki iliyopita, watu 12,900 walipatwa na homa ya dengue huku wengine 20 wakifariki, na watu 12 zaidi walifariki kwa ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo (meningitis), kwa mujibu wa Wizara ya Afya.