1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kirusi cha Omicron chazusha taharuki ulimwenguni

29 Novemba 2021

Mawaziri wa Afya wa Kundi la mataifa tajiri ulimwenguni la G7 wanatarajiwa kufanya mkutano wa dharura leo kuhusu aina mpya ya kirusi cha Covid-19 cha Omicron ambacho kinasambaa ulimwenguni na kulazimisha kufungwa mipaka

Neue COVID-Variante in Südafrika
Shughuli zimevurugika baada ya safari za ndege kufutwaPicha: Jerome Delay/AP/picture alliance

Mkutano huo umeitishwa na mwenyekiti wa G7 Uingereza, ambayo ni miongoni mwa idadi inayoongezeka ya nchi zinazogundua visa vya aina hiyo mpya ya kirusi kilichobadilika kabisa.

Kirusi cha Omicron, ambacho kiligunduliwa kwa mara ya kwanza kusini mwa Afrika, kinatoa changamoto mpya kwa juhudi za kimataifa za kupambana na janga la corona. Nchi kadhaa zimetangaza upya vizuizi ambavyo wengi walitumai kuwa wasingeviona tena. Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema muda unayoyoma na watu lazima wachanjwe kwa wingi. "Kwa sababu hatujui mengi kuhusu kirusi hiki, lakini ni kirusi cha kutia wasiwasi, na wanasayansi na watengenezaji dawa wanahitaji wiki mbili hadi tatu kuwa na picha kamili ya ni kwa kiasi gani kirusi hiki cha Omicron kimebadilika." Amesema Ursula.

Von der Leyen asema Omicron kinaleta wasiwasi mkubwaPicha: PETRAS MALUKAS/AFP

Orodha ndefu ya nchi tayari zimeweka marufuku ya kusaifiri kusini mwa Afrika, zikiwemo Qatar, Marekani, Uingereza, Indonesia, Saudi Arabia, Kuwait na Uholanzi.

Angola ilikuwa nchi ya kwanza ya kusini mwa Afrika kusitisha safari zote za ndege kutoka majirani wake wa kikanda Msumbiji, Namibia na Afrika Kusini. Afrika Kusini imedai kuwa inaadhibiwa kwa kukigundua kirusi hicho cha Omicron, huku Rais Cyril Ramaphosa akitoa wito kwa mataifa kuondoa marufuku za safari za ndege kabla ya uharibifu zaidi kutokea kwenye uchumi wa nchi zilizoathirika. "Kuzuia kusafiri, nchi tajiri za ulimwengu zinahitaji kuunga mkono juhudi za nchi zinazoendelea, kupata na kutengeneza dozi za kutosha za chanjo kwa watu wao bila kuchelewa." Amesema Ramaphosa. 

Soma pia: Shirika la ndege la Qatar lawapiga marufuku abiria kutoka Afrika Kusini

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amezituhumu nchi za Magharibi akisema "zina hofu dhidi ya Afrika” kwa kufunga mipaka yao. Mkuu wa SHirika la Afya Ulimwenguni barani Afrika Matshidiso Moeti pia amezihimiza nchi kufuata sayansi badala ya kutangaza marufuku za kusafiri.

Omicron iligundulika kwa mara ya kwanza Afrika KusiniPicha: Pavlo Gonchar/Zumapress/picture alliance

Maafisa wa Uholanzi wamesema waligundua visa 13 vya Omicron miongoni mwa abiria 61 waliowekwa karantini ambao waligundulika kuwa na virusi vya corona baada ya kuwasili kutoka Afrika Kusini.

Soma pia: Aina mpya ya kirusi cha Covid-19 yapewa jina la Omicron

Akizungumza wakati akimfahamisha Rais Joe Biden kuhusu kirusi cha Omicron, mwanasayansi mwandamizi wa Marekani Anthony Fauci amesema anaaendelea kuamini kuwa chanjo zilizopo sasa zinaweza kutoa kiasi Fulani cha kinga dhidi ya visa vikali vya covid.

Israel imetangaza vizuizi vikali, huku ikifunga mipaka yake kwa wageni wote – wiki nne tu baada ya kuifungua nchi kwa watalii.

Kirusi cha Omicron hata hivyo tayari kimeshapenya na sasa kinapatikana kwingineko kuanzia Uholanzi hadi Uingereza, Botswana, Hongon na Australia. Canada imekuwa nchi ya karibuni kabisa kutangaza visa vyake vya kwanza viilivyogundulika katika watu wawili waliosafiri Nigeria.

AFP