1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kishindo cha wapinzani chaubadili mkondo wa serikali Georgia

9 Machi 2023

Chama Tawala Georgia chasitisha mpango wa kuanzisha sheria inayodaiwa na wapinzani kuwa na lengo la kuzinyamazisha sauti za wakosoaji kama inavyofanyika nchini Urusi

Georgien | Proteste in Tiflis
Picha: Zurab Tsertsvadze/AP Photo/picture alliance

Nchini Georgia chama tawala kimeamua kuachana na mipango ya kuanzisha sheria yenye utata,ambayo wapinzani wanasema lengo lake lilikuwa kuzinyamazisha sauti za kuikosoa serikali.

Upinzani nchini Georgia umetoa tamko ukiapa kuendeleza maandamano yao ya kupinga kile kinachoitwa muswaada dhidi ya mawakala wa kigeni,ambao wapinzani wanaufananisha na sheria inayotumika Urusi kuwanyamazisha wakosoaji wa serikali mjini Moscow.

Tamko la upinzani limekuja licha ya chama tawala hii leo kutangaza kwamba limesitisha mpango wa kuianzisha sheria hiyo.

Vyama vya upinzani vinasema ikiwa hakuna hakikisho kwamba serikali ya Georgia itajikita kikamilifu kufuata mwelekeo wa nchi za Magharibi  basi maandamano yao yataendelea na hayatosimama.

Picha: Vano Shlamov/AFP/Getty Images

Tamko hilo limetolewa na kundi la vyama vya upinzani kupitia taarifa yao ya pamoja ambayo pia imeitisha maandamano mapya leo jioni ya kudai kuachiliwa waandamanaji chungunzima wanaoshikiliwa.

Uamuzi wa chama tawala umefuatia maandamano makubwa yaliyoitikisa nchi wiki hii.Wasiwasi umekuwa ukiongezeka kwamba Georgia iliyowahi kuwa chini ya muungano wa Kisoviet ambayo inapania kujiunga na Umoja wa Ulaya pamoja na jumuiya ya kujihami NATO, inachukua zaidi mwelekeo wa siasa za kiimla na kuendelea kubakisha mahusiano na Urusi.

Marekani ni miongoni mwa wakosoaji wa sheria hiyo kutoka jumuiya ya Kimataifa.Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Ned Price pamoja na kuitahadharisha Georgia ametowa mwito wa utulivu kwa pande zote nchini humo.

"Tunatowa mwito kwa serikali ya Georgia kuheshimu uhuru wa watu kukusanyika kwa amani na maandamano ya amani. Tunatowa mwito kwa pande zote kujizuia na kujiepusha na vurugu au machafuko lakini pia kuheshimu utawala wa sheria na misingi ya kidemokrasia ya Georgia''

Kwa siku mbili mfululizo wiki hii yameshuhudiwa maandamano makubwa ikiwemo hapo jana katika mji mkuu Tbilisi ambapo polisi walilazimika kutumia mabomba ya maji na gesi ya kutowa machozi kuwatawanya maelfu ya waandamanaji.

Picha: Zurab Tsertsvadze/AP Photo/picture alliance

Maelfu walikusanyika mbele ya bunge la nchi hiyo katikati ya mji mkuu wakiwa wamebeba bendera ya nchi na ile ya Umoja wa Ulaya wakiimba kwamba hawaitaki sheria ya Urusi. 

Baada ya kuuondowa muswaada huo, Chama tawala nchini humo kilitoa taarifa kikisema muswaada huo umetafsiriwa vibaya kwa lengo la upotoshaji na kwamba kitaanzisha mashauriano ili kutoa kile ilichokiita ufafanuzi bora kuhusu muswaada huo.

Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Georgia umeipongeza hatua ya kuusimamishwa muswada huo na kusema kwamba wanawatia shime viongozi wote wa kisiasa nchini humo kurudisha tena mageuzi yenye mwelekeo wa kuegemea upande huo wa Umoja wa Ulaya.

 

Muswaada wa sheria inayopingwa inalenga hasa kuyalazimisha mashirika yanayopokea ufadhili kutoka nje kuweka wazi ufadhili wanaopata.

Lakini wakosoaji wanasema ni sheria ambayo haitofautiani na ile inayotumika nchini Urusi kuvilazimisha vyombo vya habari na makundi ya wakosoaji kufunga shughuli zao.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW