1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kithure Kindiki ala kiapo cha unaibu rais Kenya

1 Novemba 2024

Hatimaye, Kenya inafungua ukurasa mpya kisiasa baada ya kupata naibu mpya wa rais ambaye ni Profesa Kithure Kindiki aliyekuwa waziri wa usalama wa taifa.

Naibu rais mpya Kithure Kindiki akila kiapo
Naibu rais mpya Kithure Kindiki akila kiapoPicha: Brian Inganga/AP/picture alliance

Kindiki ameapishwa rasmi Ijumaa(01.11.2024) kuwa naibu wa rais wa tatu baada ya Rigathi Gachagua kutimuliwa katikati ya mwezi Oktoba kwa makosa ya ufisadi, kukiuka katiba na matumizi mabaya ya madaraka. Haya yanajiri baada ya jopo la majaji watatu kuondoa kikwazo jana kilichozuwia naibu wa rais mpya kuapishwa.

Profesa Kithure Kindiki amekula kiapo cha kutimiza majukumu yake ya naibu wa rais kwa uadilifu. Kithure Kindiki aliahidi kutenda kazi kwa uwezo wake wote na kusisitiza kuwa yeyote anaweza kufika kokote maishani kwa uwezo wa Maulana pasina kujali historia.

Msajili mkuu wa idara ya mahakama Winfrida Mokaya akiungwa mkono na Jaji mkuu Martha Koome ndiye aliyemuapisha Profesa Kithure Kindiki kwa kufuata utaratibu wa katiba.  Shughuli hiyo ilianza rasmi saa tano kasoro dakika 18 kwenye uwanja wa jengo la mikutano la kimataifa la KICC lililoko katikati ya jiji la Nairobi.Nyimbo za kitamaduni zilisikika mjini ili kusherehekea hatua hii mpya.

Rais wa Kenya William Ruto(kushoto) akimkabidhi katiba naibu rais mpya Kithure KindikiPicha: Brian Inganga/AP/picture alliance

Usalama uliimarishwa na maeneo yaliyo karibu na KICC kuwa na ulinzi mkali. Kithure Kindiki alisindikizwa na mkewe Dr Joyce Gatiria Kithure ambaye amekuwa akimuunga mkono kila wakati katika safari yake ya kisiasa.

Soma: Mahakama Kenya yaondoa agizo la kupinga kuapishwa Kindiki

Rais William Ruto aliyesindikizwa na mama wa taifa Rachel Ruto aliwakumbusha wakenya kuwa azma yao ni kuwahudumia na wala sio kuendekeza ubinafsi kwani,”Nakuaminia ndugu yangu. Naamini utakuwa msaidizi mwema kwangu kwani nimekuwa mpweke uongozini kwenye afisi ya juu zaidi.Ninatumai yote yaliyonipita katika miaka miwili iliyopita utaweza kulijaza pengo.” alisisitiza.

Wakenya wataka huduma na kazi ifanyike

Hafla hii iliwaleta pamoja pia viongozi wa ngazi ya juu serikalini wakiwemo spika wa bunge la taifa na baraza la senate kadhalika mawaziri na mabalozi wa nchi za kigeni. Ifahamike kuwa leo imetengwa kuwa siku ya mapumziko.

Je,Wakenya wanasemaje kuhusu mwanzo huu mpya? David Mathenge ni mkaazi wa Nyeri na anaamini kuwa uamuzi wa mahakama uko sahihi kwani tulichotaka ni haki itendeke kwahiyo tuko sawa,” anamalizia.Rigathi Gachagua asema ulinzi wake umeondolewa

Profesa Kithure Kindiki aliye na umri wa miaka 52 amekuwa mwandani wa rais kwa zaidi ya muongo mmoja tangu William Ruto alipokuwa mbunge wa Eldoret North na alipoandamwa na kesi dhidi ya ubinadamu kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, ICC iliyoko The Hague, Uholanzi.

Naibu rais mpya wa Kenya Kithure Kindiki na mkewe Joyce KithurePicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Genesis Ngunjiri ni mkaazi wa Othaya na anaamini kuwa ,”mahakama iko sahihi na tumeitikia wito. Kwa vile Kindiki anatokea eneo la Mlima Kenya basi hatuna wasiwasi.Achape kazi tu.”anaeleza.

Kindiki alichaguliwa kuwa Seneta wa kaunti ya Tharaka Nithi katika uchaguzi wa mwaka 2012, nafasi aliyoishikilia hadi 2022.Katika kipindi hicho alihudumu kama mwakilishi wa chama tawala katika baraza la Senate,naibu spika na hatimaye kutemwa wakati rais mstaafu Uhuru Kenyatta alipokuwa akisafisha chama cha Jubilee.

Viongozi wengine wana mtazamo upi kuhusu utendaji wa naibu mpya wa rais Kithure Kindiki? Cecily Mbarire ni gavana wa kaunti ya Embu iliyo jirani na Tharaka Nithi anakotokea Kithure Kindiki na mwenyekiti wa kitaifa wa chama tawala cha United DemocratiC Alliance, UDA na anasisitiza kuwa,”Ijapokuwa Kindiki anaotokea eneo la Mlima Kenya, yeye ni naibu wa rais wa wakenya wote kwahiyo tumuunge mkono ili aweze kutuhudumia sisi sote.”anaasa.Mahakama yasikiliza pingamizi la kuenguliwa kwa Gachagua Kenya

Atakachopambana nacho anapoanza majukumu ya naibu wa rais ni kusafisha jina lake ukizingatia utendaji wa Profesa Kindiki aliyekuwa waziri wa usalama wa taifa uliingia doa pale serikali kuu iliponyoshewa kidole cha lawama baada ya maandamano ya kupinga gharama za maisha kusababisha maafa.

Kindiki Kithure aapishwa kuwa Naibu Rais wa Kenya

00:50

This browser does not support the video element.