1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha baa la njaa Sudan Kusini

8 Desemba 2017

Zaidi ya watu milioni 1.2 katika nchi iliyokumbwa na vita ya Sudan Kusini wananyemelewa na baa la njaa  - mara mbili zaidi ya wakati kama huu mwaka jana.

Südsudan Hunger Symbolbild
Picha: picture alliance/ZUMA Press/M. Juarez Lugo

Kulingana na mkuu wa shughuli za msaada wa kibinaadamu za Umoja wa mataifa, mwanzoni mwa mwaka 2018 nusu ya idadi ya watu nchini Sudan Kusini wataishi kwa kutegemea msaada wa dharura wa chakula.

Mark Lowcock ameliambia Baraza la Usalama la umoja wa mataifa kwamba pamoja na watu milioni mbili kuikimbia nchi hiyo zaidi ya miaka minne iliyopita, watu milioni 7 waliosalia "karibu theluthi mbili ya idadi iliyobaki" - bado wanahitaji misaada ya kibinadamu.

"Msimu unaofuata kuanzia mwezi Machi huenda tukaanza kuona  hali ya kuwepo njaa katika maeneo kadhaa nchini kote kwahiyo tunapaswa kuhakikisha tunaepuka marudio ya hali hii ambayo iliwahi kushuhudiwa na kukabiliwa" Lowcock alisema.

Jean-Pierre Lacroix, mkuu wa shughuli za kulinda amani wa umoja wa mataifa Picha: picture-alliance/dpa

Mkuu wa shughuli za kulinda amani wa umoja wa mataifa Jean-Pierre Lacroix aliitaja hali ya usalama nchini Sudan Kusini "kuwa ya hatari" na kuonya kuongezeka kwa migogoro ya kijeshi na mapigano ya kikabila wakati msimu wa kiangazi unapoingia.

Alitoa mfano mpya wa kuzuka tena mapigano kwenye jimbo la kusini la Unity katika wiki mbili zilizopita kati ya vikosi vya upinzani, washirika wa Makamu wa Rais wa zamani Riek Machar na Makamu wa kwanza wa rais wa sasa  Taban Deng.

Aidha, alisema, ukiukwaji wa haki za binadamu unaohusiana na migongano unaendelea ikiwa ni pamoja na uporaji, nyumba kuteketezwa, raia kuuawa, kukamatwa kiholela na unyanyasaji wa kijinsia, "pamoja na makundi ya wanajeshi na waasi yakihusishwa katika vita hivyo."

Lacroix alitoa wito kwa Baraza la Usalama "kuwa waangalifu na kujitahidi zaidi kulaani na kuisitisha vurugu, kulinda raia na kwa haraka kurahisisha upatikanaji wa suluhisho la kisiasa."

Machafuko Sudan Kusini mwaka wa 2014Picha: Reuters

Kulikuwa na matumaini makubwa kwamba Sudan Kusini itakuwa na amani na utulivu baada ya uhuru wake kutoka nchi jirani ya Sudan mwaka 2011.

Lakini taifa hilo  jipya zaidi ulimwenguni liliingia katika vita vya kikabila mwezi Desemba 2013 wakati vikosi vinavyomuunga mkono Rais Salva Kiir, kutoka kabila la Dinka, vilipoanza kupigana na wafuasi wa Machar,  ambaye ni wa kabila la nuer ambaye sasa anaishi Afrika Kusini.

Mkataba wa amani wa Agosti 2015 haujazuia mapigano, na vita mwezi Julai 2016 kati ya wafuasi wa Kiir na Machar yakichochea vurugu zaidi. Mgogoro huo umeua  maelfu ya watu.

Lacroix ameunga mkono kufufuliwa kwa mchakato ulioanzishwa na na shirika la maendeleo la nchi za Mashariki mwa Afrika IGAD ambalo linalenga kufikia mkataba wa kusitisha, kutekeleza makubaliano ya amani ya 2015 na kuanzisha "ratiba ya halisi ya utekelezaji wake."

Mwandishi: Fathiya Bayusuf/APE

Mhariri:Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW