1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, raia wa kanda ya Sahel wamekosa imani na demokrasia?

3 Agosti 2023

Onyo la mataifa jirani na Niger dhidi ya uingiliaji wowote wa kijeshi wa jumuiya ya ECOWAS nchini humo linatuma salamu kwa jumuiya hiyo kwamba huenda sasa mambo hayako tena kama yalivyokuwa miaka ya nyuma.

General Abdourahmane Tiani
Jenerali Abdourahmane Tiani, kulia mkuu mpya wa nchi ya Niger akiwa na viongozi wa mapinduzi mjini Niamey.Picha: REUTERS

Kitisho cha mataifa jirani ya Niger kwamba yatachukulia hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya utawala mpya wa Niamey kuwa ni uvamizi dhidi yao, kinatuma salamu kwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, kwamba huenda sasa mambo hayako tena kama yalivyokuwa miaka ya nyuma, kama utafiti wa hivi karibuni wa Umoja wa Mataifa ulivyoonesha kuwa raia wa ukanda wa Sahel wanaelemea kuwaamini zaidi wanajeshi kuliko watawala wa kiraia kuwapatia suluhisho la hali ngumu ya maisha na mashambulizi ya kigaidi.

Inavyoonekana si kila mtu anayachukia mapinduzi ya kijeshi nchini Niger na mataifa mengine ya Afrika ya miaka ya hivi karibuni, licha ya kuleta khofu kwenye mataifa ya Magharibi na washirika wao.

Kamishna wa Masuala ya Kisiasa, Amani na Usalama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Balozi Abdel-Fatau Musah (kushoto) na Mkuu wa Majeshi wa Nigeria, Jenerali Christopher Musa (Kulia) wakihutubia Wakuu wa Majeshi wengine wa ECOWAS, wakati wa mkutano. Mkutano wa ajabu huko Abuja, Nigeria kuhusu machafuko ya kisiasa katika Jamhuri ya Niger mnamo Agosti 2, 2023.Picha: KOLA SULAIMON/AFP

Katika picha ya pamoja kwenye mkutano wa kilele wa Afrika na Urusi wiki iliyopita, Rais Vladimir Putin wa Urusi anaonekana amesimama karibu na Ibrahim Traore, afisa wa jeshi kijana aliyechukuwa madaraka nchini Burkina Faso mwezi Septemba.

Soma pia: Mtawala wa kijeshi Niger aonya dhidi ya uingiliaji wa kigeni na kuutaka umma kuilinda nchi

Alipoisambaza picha hiyo kwenye mtandao wa X, katibu mkuu wa wizara ya mambo ya kigeni ya Kenya aliambatanisha na ujumbe unaosomeka: "Kuyarasimisha na kuyatukuza mapinduzi ya kijeshi barani mwetu kunapaswa kuliudhi bara letu tukufu."

Sasa serikali za kijeshi za Burkina Faso na Malizimechukuwa hatua isiyo ya kawaida kwa kutangaza kwamba uingiliaji kati wa nje dhidi ya serikali mpya ya kijeshi ya Niger utachukuliwa kuwa ni tangazo la vita dhidi yao pia.

Kauli hiyo ilikuwa ni kuijibu Jumuiya ya Uchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS, ambayo ilikuwa imetishia kutumia nguvu endapo viongozi wa kijeshi wa Niger hawatamrejesha madarakani rais aliyechaguliwa kidemokrasia, Mohamed Bazoum, ndani ya wiki.

Guinea, ambayo pia inatawaliwa na wanajeshi, ilitowa tamko tafauti kuunga mkono utawala mpya kijeshi wa Niger na kuitaka ECOWAS "kutumia akili."

Jumuiya ya Kimataifa yalaani mapinduzi nchini Niger

02:12

This browser does not support the video element.

Utetezi wa tawala hizi za kijeshi kwa kile kilichotokea Niger unakinzana na kauli ya mataifa mengine duniani na wakati huo huo kuutia majaribuni uwezo wa washirika wa ECOWAS.

Raia wana imani kubwa na jeshi kuliko watawala wa kiraia

Vile vile kinaakisi kile kilichogunduliwa na utafiti uliofanywa na Umoja wa Mataifa baada ya kuzungumza na maelfu ya raia wa nchi za Kiafrika zilizokumbwa aidha na mapinduzi ya kijeshi au mabadiliko ya serikali kupitia njia zisizo za kidemokrasia hivi karibuni.

Ripoti ya utafiti huo ilisema kwamba kuna uwezekano wa tawala za kijeshi za Mali, Guinea na Burkina Faso kushirikiana dhidi ya hatua yoyote ya ECOWAS ambayo ina mazowea ya kuingilia kati pale mapinduzi ya kijeshi yanapotokea. 

Ripoti hiyo ilionya pia kwamba tawala hizo za kijeshi zinaweza kukiuka vikwazo na kusimama kwenye chaguzi kwa msaada wa washirika wapya ya kimataifa.

Soma pia: Ujumbe wa ECOWAS watua Niger kutafuta suluhu

Ilichogunduwa ripoti hiyo kwa kiwango cha raia ni kwamba mapinduzi ya kijeshi yanaungwa mkono na umma na hivyo kuyafanya kuwa mbadala bora zaidi kwa njia za kidemokrasia kuweka na kuondowa serikali, ambalo baada ya miongo zaidi ya mitatu, wananchi hawaliamini tena.

Vijana wa Niger wakiandamana mjini Niamey kuunga mkono mapinduzi ya kijeshi. Utafiti wa Umoja wa Mataifa unaonyesha raia wengi wa Sahel wanazidi kuwaamini wanajeshi kuliko watawala wa kiraia.Picha: Fatahoulaye Hassane Midou/AP/picture alliance

Mataifa haya ya Afrika yana idadi kubwa zaidi ya vijana waliochanganyikiwa na hali ngumu ya maisha wanayoamini inachangiwa na mifumo ya kisiasa na kiuchumi. Vijana hawa wanashinikiza mageuzi makubwa na ya haraka ambayo hayawezi kuletwa na chaguzi za kila baada ya miaka minne ama mitano.

Soma pia: Mali, Burkina Faso zaonya dhidi ya uingiliaji wa kijeshi nchini Niger

Wengi wa vijana hawa wanataka wajisikie salama katika nchi zao wakati huu makundi ya siasa kali yakijitanuwa kwenye ukanda wa Sahel. Kama anavyosema raia mmoja wa Mali anayeishi sasa nchini Guinea, Harber Cisse, utawala wa kijeshi wa Niger, unaweza zaidi kuunganisha nguvu zao na wa Mali na Burkina Faso kupambana na ugaidi.

Kwa Cisse, kama ilivyo kwa wananchi wengi wa ukanda wa Sahel, anaamini kuwa watawala kama Rais Mohamed Bazoum wamekuwa wakijitia upofu na kuyaacha makundi ya siasa kali kuingia kutokea Mali.