1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha Ebola DRC

Oumilkheir Hamidou
7 Desemba 2018

Kitisho cha maradhi ya Ebola katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na dhana dhidi ya kutumiwa vibaya misaada kwaajili ya wakimbizi nchini Uganda ni miongoni mwa yaliomo katika magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika

Ebola im Kongo
Picha: picture-alliance/dpa/A.-H.K. Maliro

Tunaanzia jamahuri ya kidemokrasi ya Kongo ambako zaidi ya watu 400 wanasemekana wameambukizwa virusi vya maradhi ya Ebola. Kutokana na janga hilo , hatua za kupambana na ebola zinaonekana kana kwamba hazisaidii kitu linaandika gazeti la kusini mwa Ujerumani Süddeutsche Zeitung. Gazeti limemnukuu Richard Kitenge wa wizara ya afya akisema "wamefikia ukingoni"."Sisi ni raia na sio wanajeshi" ameendelea kusema. Hii ni mara ya pili katika kipindi cha mwaka mmoja kwa Richard Kitenge kukabiliana na kishindo cha maradhi hayo yanayouwa ya Ebola. Zaidi ya watu 425 wameambukizwa virusi vya Ebola na zaidi ya wengine 240 wamefariki dunia tangu maradhi hayo yaliporipuka mapema mwezi wa Agosti mashariki mwa Kongo Süddeutsche Zeitung linayataja maradhi hasyo kuwa mabaya zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo na ya pili makubwa zaidi ulimwenguni. Wizara ya afya ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na pia mashirika ya kimataifa yanapata shida kubwa kuyadhibiti maradhi hayo. Gazeti linamalizia kwa kumbusha hatari ya kuenea maradhi hayo yanayoambukiza ,eneo la mashariki mwa Kongo linakumbwa na mapigano na wakaazi wengi wanakimbilia katika maeneo mengine kutafuta usalama, linasema Süddeutsche Zeitung.

Wimbi wa wakimbizi nchini UgandaPicha: Reuters/J. Akena

Wakimbizi ni tatizo jengine kubwa linalozikumba nchi za Afrika na Uganda, kwa mujibu wa gazeti la mjini Berlin, die tageszeitung ndio inayowapokea wakimbizi wengi zaidi kuliko nchi yoyote nyengine barani Afrika. Sera yake ya kiliberali kuhusu wakimbizi inasifiwa na jumuia ya kimataifa. Sasa lakini Uganda inatuhumiwa kuhusika na visa vya udanganyifu kuhusiana na wakimbizi: gazeti la die tagesteitung linazungumzia kuhusu idadi bandia ya wakimbizi walioorodheshwa, misaada inayotumiwa vibaya na madai hayo yamethibitika katika uchunguzi uliosimamiwa na Umoja wa mataifa. Uchunguzi huo unawatwika jukumu la rushwa na wizi maafisa  wa serikali ."NI kashfa kubwa hii inayoizonga nchi iliyokuwa ikipigiwa mfano katika kuwapokea wakimbizi-Uganda" limeandika Die Tageszeitung na kunukuu  ripoti ya uchunguzi uliosimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi UNHCR.Tuhuma za rushwa zilisikika tangu mapema mwaka huu dhidi ya wizara inayoshughulikia masuala ya waakimbizi nchini Uganda. die tageszeitung limzungumzia onyo lililotolewa wakati ule na kamishna wa shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia wakimbizi Filippo Grandi  pindi dhana hizo zikithibitika. Zimethibitika na rushwa inaonyesha imeota mizizi" linaandika gazeti la die tageszeitung. Kutoka jumla ya wakimbizi milioni moja na laki nne waiorodheshwa,,zaidi ya laki tatu ni bandia. Idadi hiyo kubwa ya waakimbizi ndio iliyopelekea gharama za shirika la Umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR kwa Uganda kuongezeka mwaka 2017 na kupindukia dala milioni 200-sehemu kubwa ya fedha hizo ikitolewa na nchi za umoja wa ulaya, Ujerumani, Uingereza na Marekani limemaliza kuandika gazeti la Die Tageszeitung.

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inatupeleka kusini mwa bara lam Afrika, nchini Zambia, nchi yenye utajiri wa maadini ya shaba lakini wakaazi wake wanaishi katika hali ya umaskini. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaandika kuhusu hasira za wakaazi wa nchi hiyo kutokana na ushawishi mkubwa wa China inayosemekana inakurubia kudhibiti shirika la nishati la nchi hiyo. Hisia za fakhari walizokuwa nazo wananchi wa Zambia baada ya kupata uhuru kutoka Uingereza mwaka 1964, zimetoweka  Takriban kila kitu hivi sasa kinadhibitiwa na wachina,amenukuliwa Boniface Cheembe, naibu mweyekiti wa taasisi ya kutatua mizozo ambae pia ni profesa katika chuo kikuu cha Lusaka akilalamika na kufika hadi ya kusema wazambia walio wengi wanatamani wakoloni wa kiingereza wangerejea.

Na kwa ripoti hiyo ya Frankfurter Allgemeine ndio tunaufunga ukurasa wa afrika katika magazeti ya ujerumani wiki hii.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/presse

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW