Kitisho cha kurejea enzi za vita baridi ulimwenguni
6 Desemba 2018Tunaanza na kitisho cha kuanza upya mbio za kujirundukia silaha zilizoshuhudiwa katika enzi za vita baridi. Viongozi wa Marekani wameipa muda wa siku 60 Urusi ikongowe mfumo wa makombora chapa 9M279 yanayoweza kuhamishwa toka eneo moja hadi jengine la sivyo watajitoa katika makubaliano ya mwaka 1987 yanaopiga marufuku makombora ya masafa ya wastani yenye uwezo wa kushambulia umbali wa kilomita 500 hadi 5500. Gazeti la Oberhessische Presse linaandika: "Wiki chache kutoka sasa wamarekani na warusi wanaweza kuyazika makubaliano hayo ya kupunguza silaha za nuklea. Kwa namna hiyo, katika sera za usalama nchi za ulaya zitajikuta zikirejeshwa katika enzi za miaka ya 80. Kama ilivyokuwa kabla ya ukuta wa chuma kuporomoka, watu watalazimika kuishi kwa hofu Moscow au Washington wasije wakabonyeza kifungo chekundu na kuzusha vita vikuu vya tatu vya dunia.
Hakuna yeyote mwenye busara anaeweza kutarajia hali kama hiyo. Lakini wanamikakati wa kijeshi mijini Moscow na Washington hawawezi kuingizwa katika mkumbo huo. Wanaendelea kuamini kuhusu tiba ya kitisho cha nuklea. Marekani na Urusi wanatupiana lawama ya kutaka kusababisha mwisho wa mkataba unaopiga marufuku silaha za nuklea-INF. Hatuhitaji kuwa wataalam wa masuala ya kijeshi kugundua wote wawili wananyunyizia mafuta ."
Msako dhidi ya wahalifu wa Ndrangheta katika nchi tofauti ulimwenguni
Msako wa kimataifa dhidi ya wahalifu wa kundi kubwa kabisa la Mafia la Italia, "Ndrangheta" umeripotiwa katika nchi tofauti za dunia. Biashara ya madawa ya kulevya inawapatia wahalifu hao mabilioni ya fedha kwa mwaka. Gazeti la Badische Zeitung linasifu ushirikiano wa kimataifa katika msako huo na kuandika: "Kwamba vyombo vya sheria katika nchi za Umoja wa ulaya vimeshirikiana katika kuandaa opereshini hiyo ni ushahidi wa umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kupambana na makundi ya wahalifu waliojiandaa. Umuhimu kama huo unakutikana pia nchini Ujerumani.
Mauwaji yaliyofanywa na wahalifu wa mafia mwaka 2007 katika mji wa Duisburg yamedhihirisa jinsi Mafia walivyopiga kambi katika baadhi ya majimbo humu nchini. Na hawako peke yao. Wanashindana na makundi ya wahalifu kutoka bandi za muziki wa rock na pia baadhi ya koo kutoka nchi za kiarabu na nchi za Ulaya ya mashariki. Italia imezidisha makali ya sheria zake dhidi ya Mafia miaka ya hivi karibuni, Ujerumani inangojea nini?"
Nani atamrithi Angela Merkel kama mwenyekiti wa CDU?
Mada yetu ya mwisho magazetini inatupia jicho mkutano mkuu wa chama cha Christian Democratic Union mjini Hamburg. Lengo ni kumchagua atakaemrithi Angela Merkel kama mwenyekiti wa chama hicho. Gazeti la Westfalenpost linaandika: "Wajumbe hawatakuwa na kazi rahisi. Bila ya kuzingatia matokeo ya mashindano hayo ya kisiasa, mtu anaweza kusema mgombea aliyejitangaza upesi upesi amezidisha mori katika majadiliano yanayoendelea. Mikutano ya kimkoa yamekipatia ushindi chama cha CDU. Wanavuliwa kofia mpaka nje ya chama chao. Na sio tu kwasababu Friederich Merz ameahidi kujitosa ringini dhidi ya Chaguo Mbadala kwa Ujerumani AfD."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri-Yusuf Saumu