Kitisho cha kuzidi kuenea Malaria barani Afrika
4 Desemba 2019Fedha za kugharamia mapambano jumla dhidi ya malaria, maradhi yanayouwa mtoto mmoja kila dakika mbili, zimekwisha , linaonya shirika la Afya la Umoja wa Mataifa-WHO, na kwakua mbu ndio chanzo cha kuenea maradhi hayo basi kuna uwezekano kuona nusu ya idadi ya wakaazi wa dunia wakikabiliwa na hatari ya kushikwa na maradhi hayo.
WHO limeyatolea wito mataifa fadhili na serikali za nchi zinazoathirika na maradhi hayo wazifufue juhudi za kupambana na Malaria.
"Ulimwengu umedhihirisha maendeleo yanawezekana" amesema mtaalam wa masuala ya Malaria, Pedro Alonso mbele ya waandishi habari. Ametoa mifano ya nchi ambako kadhia za Malaria zimepungua sawa na ilivyopungua idadi ya vifo tangu mwaka 2010. Kadhia za watu wanaoshikwa na malaria zimepungua kutoka watu milioni 239 na kufikia watu milioni 214 mwaka 2015 na vifo pia vimepungua kutoka watu 607 000 hadi watu laki tano mwaka 2013.
Juhudi za kupambana na malaria zinadorora
Kadhia za walioshikwa na Malaria zimepungua kidogo tu mwaka 2018 kutoka watu milioni 231 mwaka 2017 na kufikia watu 228, na watu 416 000 waliokufa mwaka 2017 waakilinganishwa na watu 405.000 waliokufa mwaka jana.
Ripoti ya shirika la Afya la Umoja wa mataifa WHO inasema wanawake wajawazito na watoto barani Africa wanaendelea kuvumilia kishindo cha maradhi ya malaria.
Wanawake wajawazito wanaokadiriwa kufikia milioni 11 wanaoishi katika eneo la Africa Kusini mwa jangwa la Sahara-kiwango ambacho ni sawa na asili mia 29 ya wanawake wote wajawaziito wa kanda hiyo- wameshikwa na malaria mwaka 2018, na kupelekea watoto karibu laki tisa kuzaliwa na uzito mdogo kabisa kwa namna ambayo afya yao imeingia hatarini.
Zaidi ya thuluthi ya vijana wanaoishi katika kanda ya Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara hawakuwa wakilala kwenye kitanda cha chandaruwa mwaka 2018 .
Ushirika katika juhudi za kupiga vita malaria umesema ripoti ya WHO inaonyesha juhudi jumla na uwekezaji ni muhimu sana katika kuendeleza maendeleo yaliyofikiwa hadi wakati huu . Ushirika huo umezitolea wito serikali zisichzoke.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu