1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha kuzuka vita Kongo Kinshasa Magazetini Ujerumani

Oumilkheir Hamidou
2 Machi 2018

Kitisho cha kuripuka vita katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, mdajala wa bunge, Afrika kusini kuhusu kutaifishwa ardhi na mitindo ya mavazi kutoka Afrika ni miongoni mwa mada za Afrika magazetini wiki hii Ujerumani

Demokratischen Republik Kongo -  Straßenszene in Goma.
Picha: DW/F. Quenum

Tunaanzia maziwa makuu na hasa katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo ambako wataalam wanaonya dhidi ya hatari ya kuibuka vita: Chanzo linaandika gazeti la mjini Berlin, "Berliner Zeitung" ni kucheleweshwa uchaguzi na mapigano yaliyoenea katika majimbo kadhaa ya nchi hiyo. Mhariri wa gazeti hilo, Johannes Dietrich anaripoti jinsi polisi walivyokuwa wakivurumisha maguruneti na kufyetua hewa za kutoa machozi dhidi ya maandamano ya amani katika kitongoji kimoja cha mji mkuu Kinshasa, yaliyokuwa yametanguliwa na mapadri waliovalia nguo nyeupe. Katika wakati ambapo waandamanaji wengi wamekimbia, mapadri walisimama wima au kupiga magoti. Na licha ya hayo walipigwa na polisi na wale walioanguka wakakanyangwa. Berliner Zeitung linakumbusha picha kama hizi zinashuhudiwa kila kukicha katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Joseph Kabila anaonyesha hatishiki

Kwa jumla watu 20 wamepoteza maisha yao mwaka huu katika maandamano kama hayo ya amani yanayoandaliwa na kanisa, mamia wamejeruhiwa na wengine  wengi zaidi kukakamatwa. Kanisa katoliki linajihusisha sana na mzozo wa nchi hiyo, mzozo ambao kwa mujibu wa wataalamu unaweza haraka kugeuka vita. Baada ya rais Joseph Kabila kukataa kung'atuka na kuitisha uchaguzi, mhula wake wa pili ulipomalizika, miaka miwili iliyopita, kanisa ndilo lililopatanisha. Kabila lakini hakuheshimu yaliyofikiwa. Licha ya onyo  na kuzuwiliwa misaada na baadhi ya  nchi za magharibi, Kabila haregezi kamba. Berliner Zeitung linamaliza kwa kusema hata wanajeshi 18000 wa kulinda amani wa Umoja wa mataifa waliowekwa nchini humo hawamshitui seuze tena  seriklali ya Marekani inaitaka taasisi hiyo ya kimataifa ipunguze gharama.

 Mjadala wa kutaifisha ardhi bilaya fidia Afrika Kusini

Nchini Afria kusini bunge linajadiliana namna ya kukabiliana na suala la vipi wazungu wa nchi hiyo wanaweza kupokonywa ardhi wanayoidhibiti. Lilikuwa gazeti la  kusini mwa Ujerumani, Süddeutsche Zeitung lililochambua suala hilo na kusema mpaka rais mpya Cyril Ramaphosa anaiunga mkono fikra hiyo. Gazeti linasema miaka 24 baada ya kumalizika utawala wa ubaguzi wa rangi na mtengano Apartheid, bado wazungu wa Afrika kusini wanadhibiti asili mia 73 ya ardhi ya kilimo."Ingawa mwisho wa enzi za ubaguzi wa rangi na mtengano-Apartheid umewaletea uhuru wa kisiasa na usawa mbele ya vyombo vya sheria, hata hivyo katika sekta ya kiuchumi bado dhuluma inaendelea.

"Hakuna mada nyengine inayohanikiza katika jamii kama hii ya kumiliki ardhi "anaandika Tobias Zick wa gazeti hilo la mjini Munich. Süddeutsche Zeitung limemnukuu mwanasiasa wa upinzani Julius Malema, mwenyekiti wa chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto-"Economic Freedom Fighters" ( EFF) akisema bungeni mjini Capetown "Enzi za kusawazisha zimekwisha, enzi sa sasa ni za haki sawa". Chama chake cha "Wapigania uhuru wa kiuchumi" kimewasilisha mswaada wa kuifanyia marekebisho katiba kwa namna ambayo wenye kumiliki mashamba wataweza kupokonywa ardhi zao bila ya kulipwa fidia.

Mitindo ya kiafrika na  vijana wa Afrika

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inatupeleka katika ulimwengu wa mitindo . Jarida la Super Illu linazungumzia jinsi mwanafunzi kijana wa Rwanda, Paul Böger, mwenye umri wa miaka 22 alivyofanikiwa kutengeneza kitambulisho chake mwenyewe cha mitindo au labo, anayoiita "Izuba" au "juwa" kwa kiswahili, kutokana na  kuvutiwa na vitambaa vya rangi rangi vya kiafarika. Jarida la Super Illu linasema ikiwa vijana wanaanza kwa kujipatia mafunzo, na baadae kufungua viwanda au biashara zao, Paul Böger ameanza vyengine kabisa. Amebuni lebo, akafungua duka lake mtandaoni na baadae ndipo alipoanza kusomea uchumi katika shule ya masomo ya juu ya Jena. Jarida la Super Illu linasifu kipaji cha kijana huyo anaeishi katika mji wa Darmstadt na kusema mitindo yake inawavutia wengi, kuanzia  Ujerumani, kupitia Austria, Ubeligiji na kwengineko. Kila mtindo mmoja unaponunuliwa, Euro moja inaingia katika fuko la kuwahudumia watoto wa familia zisizojimudu nchini Rwanda.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/ siehe DW, Pressedatabank / und Anna Bakovic

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW