Kituo cha Corona chateketezwa Congo,
17 Juni 2020
Vijana hao wa mtaa wa Bagira waliandamana barabarani kuonesha hasira yao baada ya kijana wa kiume mwenye umri wa miaka ishirini na mbili kupigwa risasi na kupoteza maisha papo hapo usiku wa kuamkia Jumanne.
Vijana hao walisema kwamba mwenzao alipigwa risasi kwa vile polisi walimkuta hajavaa barakoa. Marko Asani ni miongoni mwa vijana waliokuwa wakiandamana.
Waandamanaji walifunga barabara wakati wakiandamana
Huyo ni mtu wa pili kuuawa baada ya kijana mwingine kufyatuliwa risasi na polisi katika kata ya Chai ndani ya mtaa huo huo wa Bagira wiki moja iliyopita. Kiongozi wa shirika la kiraia katika mtaa wa Bagira, Gentil Kulimushi amelaani vitendo vya unyanyasaji na mauaji wanavyokuwa wahanga wakaazi wa Bukavu wakati huu mgumu wa janga la virusi vya corona, na anaitaka polisi ioneshe uzalendo katika kuifanya kazi yake.
Waandamanaji hao wenye hasira kubwa waliweka vizuizi barabarani, na baadae walikishambulia kituo kinachowahifadhi wagonjwa wa virusi vya corona katika eneo la Bwindi na kuvunja vioo vya nyumba kwa mawe.
Baadhi ya watu walioshuhudia wana hofu kwamba kwamba kuna uwezekano kuwa wagonjwa wa virusi vya corona walitoroka wakati huo ili kuokoa maisha yao wakati wa shambulizi hilo.
Ila tangazo moja la gavana wa mkoa wa Kivu Kusini, Théo Ngwabidje linakanusha hoja hizo na kuhakikisha kwamba wagonjwa wote waliokuwa ndani ya kituo hicho wamebaki na sasa wanapewa huduma za matibabu kama kawaida.
Polisi imejitenga na mauaji ya kijana huyo
Pamoja na kulaani mashambulizi hayo, gavana huyo anatupilia mbali shutuma zote dhidi ya polisi na kusema kwamba wanaohusika katika mauaji ya kijana huyo ni magaidi wanaomiliki silaha na ambao hadi sasa wanatafutwa na vyombo vya usalama.
Polisi ya mji wa Bukavu pia imetupilia mbali tuhuma dhidi yake na kusema kwamba wakati wa tukio la mauaji hayo, hakuna polisi waliokuwa wakipiga doria katika eneo hilo.
Munganga Nakarhwa ni kiongozi wa kata ya Lumumba mtaani Bagira. Anawasihi wakaazi kuwa watulivu.
Polisi imefyatua mabomu ya kufuta machozi na hata pia risasi za moto ili kurejesha hali kuwa shwari, na pia kuondoa vizuizi barabarani. Kwa sasa, kumeanzishwa pia shughuli za ukarabati wa kituo cha kuhifadhi wagonjwa wa virusi vya corona kilichoathiriwa. Kulingana na takwimu husika za ufuatiliaji wa ugonjwa wa COVID-19 Kivu Kusini, mkoa huu una wagongwa 108.