1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Kituo cha mafunzo ya kijeshi Mali chashambuliwa

Hawa Bihoga
17 Septemba 2024

Jeshi nchini Mali limesema kambi yake ya mjini Mkuu Bamako imeshambuliwa mapema leo Jumanne. Hata hivyo jeshi linasema hali imedhibitiwa na usalama umeimarishwa zaidi katika eneo hilo lililoshambuliwa.

Bamako, Mali  | Wanajeshi wa jeshi la Mali
Wanajeshi wa Mali wakiwa kwenye doria kwenye moja ya kituo cha kijeshi mjini Bamako.Picha: Fabien Offner/AFP/Getty Images

Jeshi la Mali limesema hali katika mji mkuu Bamako imedhibitiwa, baada ya wapiganaji kuvamia na kushambulia chuo cha mafunzo maalum ya kijeshi cha Faladie.

Shirika la habari la Reuters linaripoti kwamba majira ya saa kumi na moja alfaji, milio ya risasi ilisikika hasa katika mitaa ya Banankabougou na kuvuruga kabisa shughuli za kiutukatika nyakati hizo, ikiwemo wale waliokuwa wanakwenda kufanya ibada.

Baadhi ya wakaazi wameripoti kwamba milio ya risasi ilirindima pia kutokea katika upande wa uwanja wa ndege.

Baadhi ya maafisa wa usalama ambao hawakutaka kutajwa majina yao walisema milio hiyo ya risasi ilianzia kusikika katika vitongoji kadhaa, ikiwa ni pamoja na maeneo ya karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa  Modibo Keita. 

Soma pia:Mali, Burkina na Niger kuanzisha pasi mpya za kusafiri za bayometriki

Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Jeshi nchini Mali Kanali Marima Sagara bila kutoa maelezo zaidi alisema amepokea taarifa ya kushambuliwa kwa kambi ya mafunzo ya gendarme mjini Bamako.

Hata hivyo haikubainika hasa washambuliaji hao waliwa wangapi lakini jeshi limesema hivi punde kwamba shambulio hilo la kigaidi limedhibitiwa naoparesheni bado inaendelea.

Mali pamoja na majirani zake Burkina Faso na Niger, kwa zaidi ya muongo mmoja wamekuwa wakipambana na uasi unaopangwa na makundi yanayomiliki silaha, ikiwa ni pamoja na washirika wa al-Qaida na kundi la dola la kiislam.

Hali ya kiusalama baada ya mapinduzi

Kufuatia mapinduzi ya kijeshi kwenye mataifa yote matatu katika miaka ya hivi karibuni watawala wa kijeshi wamevifukuza vikosi vya Ufaransa na  kuimarisha mahusiano zaidi na Urusi wakipata masaada wa kijeshi kwa kila nyanja kupitia kundi la mamluki la Wagner. Mashambulizi katikati na kaskazini mwa Mali yameshuhudiwa yakiongezeka.

Ujerumani kuisaidia Burkina Faso kupambana na uasi

01:11

This browser does not support the video element.

Mnamo mwezi Julai takriban wapiganaji 50 wa Wagner waliuwawa katika msafara ulioshambuliwa kwa kushtukiza na wanajihadi wenye mafungamano na al- Qaida na kusababisha hasara kubwa.

Soma pia:jeshi la Marekani lamaliza kuondoka Niger, baada ya mchakato ulioanza tangu ilipotakiwa kuondoka

Maelfu ya watu wameuwawa na wengine mamilioni wakiyahama makaazi yao katika maeneo hayo huku  mashirika ya kutetea haki za binadamu wakituhumu serikali na wapiganaji kwa unyanyasaji dhidi ya raia.

Mamlaka nchini humo kushindwa kurejesha hali ya utulivu na usalama katika maeneo hayo kulichangia mapinduzi mara mbili nchini Mali ikiwa ni mwaka 2020 na 2021 yakifuatiwa na mawili katika taifa jirani ya Burkina Faso na moja nchini Niger.

Hata hivyo mashambulizi ya wanajihadi yameendelea kushuhudiwa licha ya ahadi za watawala wa kijeshi kuimarisha hali ya usalama, ikiwa ni pamoja na kufukuza washirika wa magharibi kwa msaada wa Urusi kupitia Wagner.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW