Kituo cha mpakani Eres chashambuliwa Israel.
6 Machi 2004Matangazo
GHAZA CITY: Hii leo yalifanyika mashambulio mawili katika kituo cha Eres kwenye mpaka wa Israel na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Upande mmoja, wanajeshi wa Israel walimpiga risasi na kumwua mtu aliyewashambulia kutokea gari yake. Upande wa pili Mpalestina mwengine alifanya shambulio la kujiripua mwenyewe na gari yake. Inasemekana waliuawa watu wanne na kujeruhiwa watu kumi katika mripuko huo. Ili kuepusha mashambulio ya kigaidi wakati wa sherehe zake za Purim, Israel imeanza kuongeza hatua zake za usalama mnamo siku chache zilizopita. Mojawapo ya hatua walizochukua wanajeshi wa Israel ni kuzingira makao makuu ya Rais wa Wapalestina Yasser Arafat.
