1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Droni za Iran zashambulia kiwanda cha mafuta Kuwait

20 Machi 2026

Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Kuwait kimeshambuliwa na ndege zisizo na rubani za Iran.

Mwanga wa dhoruba jijini Kuwait 2026
Mwanga wa dhoruba jijini Kuwait 2026Picha: Yasser Al-Zayyat/AFP

Wakati huohuo, tahadhari za makombora zilitolewa Israel, na milipuko ilisikika mjini Tehran kutokana na mashambulizi ya Israel na kadhalika Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) wanasema mashambulizi ya Marekani na Israel yameua msemaji wao. Hayo yanafanyika katika siku ambayo Iran inadhimisha mwaka mpya wa Kiajemi.

Vita ambavyo tayari vinaathiri uchumi wa dunia vinaingia katika juma la tatu, huku Iran ikiendelea kufanya mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati katika eneo la Ghuba. Serikali ya Kuwait imethibitisha kuwa awamu mbili za mashambulizi ya droni kwenye kiwanda cha kusafisha mafuta cha Mina Al-Ahmadi zilisababisha moto ambao vikosi vya zimamoto vilikuwa wakiuzima.

Kiwanda hicho, chenye uwezo wa kusindika zaidi ya mapipa 700,000 kwa siku, kiliharibiwa pia Alhamisi katika shambulio lingine kutoka Iran ni miongoni mwa viwanda vitatu vya kusafisha mafuta nchini Kuwait, taifa dogo lakini lenye utajiri mkubwa wa mafuta. Mashambulizi ya Iran yameongezeka dhidi ya maeneo ya nishati ya mataifa ya Kiarabu baada ya Israel kushambulia eneo la gesi la South Pars liliopo baharini katika Ghuba ya Uajemi.

Taarifa ya kuuawa kwa msemaji IRGC

Na Vikosi vya Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) vimesema mashambulizi ya Marekani na Israel yamesababisha kuuawa kwa msemaji wao, Ali Mohammad Naini. Katika taarifa iliyotolewa kupitia tovuti yao ya Sepah News, vimedai kuwa Naini ameuawa katika shambulio lililofanywa alfajiri.

Msemaji wa Walinzi wa Mapinduzi Ali Mohammad NainiPicha: Tasnim

Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ameweleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Yvette Cooper, kupitia simu ingawa haijulikani ni siku gani mazungumzo yalifanyika  kwamba kama Marekani itatumia vituo vya kijeshi vya Uingereza kufanya mashambulizi dhidi ya Iran, basi Iran itachukulia Uingereza kama mshiriki wa moja kwa moja katika "uvamizi” dhidi yake.

Araghchi amesema pia kuwa ikiwa hilo litatokea, litahesabika kama tukio muhimu litakaloathiri historia ya uhusiano kati ya Iran na Uingereza.

Uhispania inakabiliana na kudhibiti bei ya mafuta

Serikali ya Uhispania inatarajiwa kutangaza kupunguza kiwango cha Kodi ya Ongezeko la Thamani VAT kwenye bidhaa za mafuta, ikishusha kutoka asilimia 21 hadi 10. Hatua hiyi ni sehemu ya mpango wa kupunguza athari za kiuchumi zinazotokana na mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati, kwa mujibu wa taarifa ya kituo cha redio cha SER kilichonukuu vyanzo vya karibu na mpango huo.

Zaidi ya hilo, serikali ya Madrid inapanga kuondoa kwa muda kodi maalum inayotozwa kwenye bidhaa za hidrokarboni. Hatua hii ingesababisha kushuka kwa bei ya dizeli na petroli kati ya euro 0.30 na euro 0.40 kwa kila lita.

China imetoa himizo la kusitishwa uhasama

China inazitaka pande zote zinazohusika katika mzozo wa Ghuba kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea bila usumbufu na kubaki thabiti. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lin Jian, akisema "Kuongezeka kwa mvutano wa sasa katika Mashariki ya Kati, huku mapigano yakiendelea kusambaa zaidi, hakuathiri tu amani na uthabiti wa eneo hilo, bali pia kunaathiri moja kwa moja nishati ya kimataifa, fedha, biashara na usafirishaji wa majini. Haya yote yanahatarisha maslahi ya pamoja ya mataifa yote. Historia na hali halisi ya sasa imeonesha mara nyingi kwamba kutumia nguvu si njia ya kutatua matatizo. Kuchagua mapambano ya kijeshi kutazalisha tu uadui mpya.”

Ama katika taarifa nadra, Kiongozi Mkuu mpya wa Iran, Ayatollah Mojtaba Khamenei, amesema kuwa maadui wa Iran wanapaswa kupoteza "usalama wao.” Hajaonekana hadharani tangu kuchukua nafasi ya baba yake, Ayatollah Ali Khamenei, aliyeuawa katika shambulio la Israel siku ya kwanza ya vita.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW