Kiwango cha maambukizi barani Afrika bado kiko chini
1 Aprili 2020Janga la virusi vya corona limeuwa watu watano na kuwaambukiza watu wengine zaidi ya 1,300 nchini Afrika kusini, waziri wa afya wa nchi hiyo amesema jana, akitoa matumaini kidogo kwamba usambaaji wa virusi hivyo sio wa kasi kama ilivyotarajiwa. Ugonjwa wa COVID-19 tayari umeshaingia Burundi, nchi ambayo kwa muda mrefu ilikuwa haijaguswa na maambukizi ya virusi hivyo. Sekione Kitojo na taarifa zaidi.
Wagonjwa wawili wamethibitika kuwa na ugonjwa huo wa COVID-19 , mmoja akiingia nchini humo akitokea Rwanda, na mwingine ni raia wa nchi hiyo ambaye aliingia nchini humo akitokea Dubai. Timu ya mawaziri na maafisa mbali mbali wa serikali wanaohusika na mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona nchini humo wanakutana wakati huu kujadili hatua zaidi za kuchukua.
Janga la virusi vya corona limewauwa watu watano nchini Afrika kusini na watu 1,353 wameambukizwa ugonjwa huo , waziri wa afya Zweli Mkhize amesema na kuongeza kwamba licha ya uchelewesho na wingi wa sampuli za damu katika huduma za maabara, watu 39,500 wamefanyiwa uchunguzi wa virusi hivyo wakati nchi hiyo inaingia katika siku ya tano kati ya siku 21 za kufungwa kabisa .
Kiwango cha ongezeko la maambukizi hakiko juu kama ilivyotarajiwa," Mkhize amesema.
Lagos mitaa iko tupu
Mji wenye wakaazi wengi kabisa barani Afrika wa Lagos umekuwa hauna watu mitaani baada ya Nigeria kuwataka wakaazi wake kubakia nyumbani na kuufunga mji huo ambao ni kitovu cha biashara nchini humo , pamoja na mji mkuu Abuja.
Katika bara la Afrika , nchi zimerekodi zaidi ya kesi 5,700 za maambukizi ya virusi vya corona na vifo 190, kwa mujibu wa idadi iliyotolewa na shirika la habari la AFP.
Idadi hiyo imekuwa ya chini ikilinganishwa na mabara mengine, na kuna baadhi ya nchi ambazo bado hazijapata mtu aliyeambukizwa.
Lakini wataalamu wamekuwa wakionya kuhusu hali tete ya Afrika , wakieleza kuhusu mizozo yake mingi, ukosefu wa maeneo ya kufanya usafi wa mwili, maeneo ya mijini yenye wakaazi wengi katika maeneo ya mabanda pamoja na hospitali ambazo hazina vifaa vya kutosha, na kusema kuna uwezekano wa kuzuka maafa makubwa.
Tanzania, Botswana na mauritania zimekuwa nchi za hivi karibuni kabisa kutangaza vifo kutokana na virusi vya corona na Sierra Leone imethibitisha mtu wa kwanza kuambukizwa.
Ethiopia imetangaza kuahirisha uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa corona. Uchaguzi huo ulionekana kama mtihani muhimu kwa ajenda za mageuzi za waziri mkuu Abiy Ahmed katika kile ambacho kilikuwa hapo kabla taifa lenye ukandamizaji mkubwa barani Afrika.